Babu Owino amjibu rais wa Uganda Yoweri Museveni

Babu alipuuzilia mbali matamshi ya Rais Museveni akisema ataendelea kuunga mkono utawala wa kidemokrasia.

Muhtasari

• Museveni alimshutumu Babu Owino kwa kujiingiza katika siasa za nchi yake,.

• Alisema alikuwa na habari za kijasusi kwamba Babu anashirikiana na upinzani nchini Uganda.

BABU OWINO
BABU OWINO

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amemjibu Rais wa Uganda Yoweri Museveni baada ya rais huyo kumshutumu kwa kuingilia siasa za nchi yake.

Babu ambaye uhusiano wake na kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine unaonekana kumkera rais Museveni alipuuzilia mbali matamshi ya Rais huyowa Uganda akisisitiza kwamba ataendelea kuunga mkono utawala wa kidemokrasia na wala sio wa kiimla.

Alilinganisha hali ya sasa ya kiuchumi nchini Kenya na ile ya nchi jirani ya Uganda akisema vijana katika mataifa hayo mawili wanahitaji viongozi wazuri na wenye maono wanaowaelewa.

“Namshukuru Rais Museveni kwa kuunga mkono azma ya Baba ya Uenyekiti wa AUC. Hata hivyo, kama kiongozi kijana nchini Kenya, baada ya kukulia katika umaskini, najua maana ya kukosa,” alisema Owino.

Katika kile kilichoonekana kama kukosoa uongozi wa rais Museveni wa takriban miaka 38, mbunge huyo alitetea haki za watu wa Uganda kupitia demokrasia, akisema kwamba Waafrika wanastahili "maono mbadala ya uongozi" ili kuwaokoa kutoka kwa ukandamizaji na umaskini.

"Kama Babu Owino, ninasimamia jamii ya kidemokrasia ambapo mtoto nchini Kenya atapokea dawa zinazofaa, na elimu na atapata kazi sawa. Vile vile, mtoto nchini Uganda anafaa kupokea matibabu sawa na ya mtoto nchini Kenya,” alibainisha.

Akizungumza katika hafla ya kuzinduliwa rasmi kwa kampeni za Raila kuwania uwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika (AUC) Museveni alimshutumu Babu Owino kwa kujiingiza katika siasa za nchi yake, akisema alikuwa na habari za kijasusi kwamba Babu anashirikiana na upinzani nchini Uganda.