Bobi Wine avunja kimya baada ya kudaiwa kujeruhiwa na polisi wa Uganda

Alisema maafisa walijaribu kuingia katika chumba chake cha hospitali ili kumnyanyasa kabla ya baadhi ya wafuasi wake kuwazuia.

Muhtasari

•Wine alidai kuwa maafisa walimfuata hadi hospitalini alikolazwa ambapo waliwahangaisha madaktari huku wakitaka rekodi zake za matibabu.

•Alieleza kwamba uamuzi wake wa kurejea nyumbani ulichangiwa zaidi na masuala ya usalama katika hospitali hiyo.

Image: TWITTER// BOBI WINE

Kiongozi wa upinzani wa Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu almaarufu Bobi Wine amelalamikia kuendelea kunyanyaswa na maafisa wa usalama wa nchi hiyo hata baada ya kudaiwa kumjeruhi siku ya Jumanne.

Katika taarifa yake Jumatano jioni, kiongozi huyo wa chama cha National Unity Platform (NUP) alidai kuwa baadhi ya maafisa walimfuata hadi hospitalini alikolazwa ambapo waliwahangaisha madaktari huku wakitaka rekodi zake za matibabu.

Pia alidai kuwa maafisa hao waliotumwa na serikali walijaribu kuingia katika chumba chake cha hospitali ili kumnyanyasa kabla ya baadhi ya wafuasi wake kuwazuia.

"Kana kwamba hiyo haitoshi, pia walifunga barabara zote zinazoelekea hospitalini, na hivyo kutatiza msongamano wa magari hospitalini na kuhatarisha maisha zaidi," Bobi Wine alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Mwimbaji huyo ambaye aligeuka kuwa mwanasiasa alifichua kuwa aliamua kwenda kuendelea na matibabu nyumbani nyumbani baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo wa mguu wake kufuatia jeraha alilopata siku ya Jumanne.

Alieleza kwamba uamuzi wake wa kurejea nyumbani ulichangiwa zaidi na masuala ya usalama katika hospitali hiyo na hali ya wagonjwa wengine waliolazwa hapo.

“Matibabu yangu yaliyosalia nitayapata kutoka nyumbani. Shukrani nyingi kwa wote mnaoendelea kutuma jumbe za fadhili na za faraja. Hivi karibuni tutazungumza,” alisema.

Hapo awali, Jeshi la Polisi la Uganda, mnamo Jumanne jioni, lilionekana kuzua shaka kuhusu madai ya kupigwa risasi kwa Bobi Wine.

Msaidizi wa Bobi Wine, Najja Ssenyonj, mapema Jumanne jioni aliibua madai kwamba kiongozi huyo wa upinzani nchini Uganda alijeruhiwa mguuni katika makabiliano na polisi aliyevalia sare.

Katika taarifa iliyosambazwa kwa umma, Jeshi la Polisi la Uganda hata hivyo lilitofautiana na madai hayo yakiashiria kwamba mwimbaji huyo wa zamani alijeruhiwa baada ya kujikwaa wakati akiingia kwenye gari lake. Haya ni kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na polisi waliokuwepo wakati wa mzozo kati ya Bobi Wine na maafisa hao.

“Leo tarehe 03 Septemba 2024, Mhe. Kyagulanyi Robert alialikwa na Bw. George Musisi (Wakili), kwa sherehe ya shukrani huko Bulindo, Manispaa ya Kiira, Wilaya ya Wakiso. Mhe. Kyagulanyi alishiriki katika sherehe hiyo, ambayo ilihitimishwa kwa amani,” taarifa ya polisi wa Uganda ilisomeka.

Wakati Mhe. Kyagulanyi aliondoka ukumbini, yeye na timu yake wakatoka nje ya magari yao na kuanza msafara wa kuelekea Bulindo mjini; hata hivyo, polisi walishauri dhidi yake.

Licha ya mwongozo wao, alisisitiza kuendelea na kufunga barabara na hivyo kusababisha polisi kuingilia kati kuzuia msafara huo. Wakati wa ugomvi uliofuata, inadaiwa alipata majeraha.

 Askari polisi waliopo eneo hilo wanadai alijikwaa wakati akiingia kwenye gari lake na kusababisha jeraha, ambapo Mhe. Kyagulanyi na timu yake wanadai kuwa alipigwa risasi,” taarifa hiyo ilisomeka zaidi.

Idara ya polisi ilisema kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli kuhusu madai mawili tofauti yaliyotolewa na pande zote mbili.