Cardinal John Njue yu hai, ripoti za kifo zathibitishwa kuwa uwongo

Askofu mkuu mstaafu Kadinali John Njue yu hai licha ya uvumi ulioenezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Muhtasari

•Kinyua alithibitisha kwamba amezungumza na askofu mkuu huyo wa zamani na akabainisha kuwa yu mzima na buheri wa afya.

•Habari za uwongo za kuaga kwa Kardinali John Njue zilienea kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii Ijumaa asubuhi.

Cardinal John Njue
Image: HISANI

Askofu mkuu mstaafu Kadinali John Njue yu hai licha ya uvumi ulioenezwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Ijumaa asubuhi.

Katika taarifa fupi Ijumaa asubuhi, askofu maarufu wa kanisa la katoliki na mwanzilishi wa CK Foundation Charles Kinyua alithibitisha kwamba amezungumza na askofu mkuu huyo wa zamani na akabainisha kuwa yu mzima na buheri wa afya.

Kufuatia hayo, Kinyua amewataka Wakenya kukoma kuenez uvumi wa kupotosha.

“Kadinali yuko vizuri. ACHENI UVUMI!! TAFADHALI. Nimezungumza naye hivi punde,” Njue alisema.

Vyanzo vingine kadhaa vya habari vya kuaminika pia vimethibitisha kwamba askofu huyo mkongwe wa kikatoliki yuko hai.

"KARDINAL NJUE YUPO HAI na MZIMA," mwanahabari Linus Kaikai alisema.

Habari za uwongo za kuaga kwa Kardinali John Njue zilienea kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii Ijumaa asubuhi na kusababisha hofu kwa wale wanaomfahamu.

Njue alijiuzulu kama askofu mkuu wa Kenya mnamo mwaka wa 2021 baada ya kufikisha umri wa kustaafu wa miaka 75.

Kanuni za kanisa zinahitaji askofu kumwandikia Papa baada ya kufikisha umri wa miaka 75 ili aruhusiwe kujiuzulu.

Nafasi ya Njue ilichukuliwa na David Kamau kama mkuu wa dayosisi ya Nairobi.

Askofu Kamau alikuwa akihudumu katika jimbo kuu kama Askofu Msaidizi wa Nairobi tangu Desemba 1999.

Njue alichukua wadhifa wa askofu wa dayosisi ya Nairobi mnamo Novemba 2007 kufuatia kustaafu kwa Ndingi Mwana Nzeki.