Dereva wa lori taabani kwa kusafirisha bangi yenye thamani ya Milioni 15 Bungoma

Muhtasari

•Dereva huyo mwenye umri wa miaka 56 alikamatwa Jumanne kando ya barabara ya Webuye-Malaba katika eneo la Pan Paper. 

•Baada ya ukaguzi wa kitaalamu kutoka kwa Idara ya Makosa ya Jinai (DCI) ilibainika kuwa thamani ya bangi hiyo ilikadiriwa kuwa Sh15M. 

Bangi ambayo ilipatikana na maafisa wa polisi.
Bangi ambayo ilipatikana na maafisa wa polisi.
Image: TONY WAFULA

Polisi katika kaunti ya Bungoma wanamzuilia dereva mmoja wa lori kwa kusafirisha gunia 10 za bangi ya uzani wa kilo 550 kutoka Uganda hadi Mombasa. 

Dereva huyo mwenye umri wa miaka 56 alikamatwa Jumanne kando ya barabara ya Webuye-Malaba katika eneo la Pan Paper. 

OCPD wa Webuye Mashariki Martha Ng'etich alisema walichukua hatua baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi.

Ng'etich alisema baada ya kupokea taarifa aliwaita maafisa kutoka Kakamega ambao walimkamata dereva huyo. 

"Baada ya polisi kukagua lori hilo walipata bangi iliyokuwa imefungwa vizuri ndani ya magunia na kumkamata dereva ambaye kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Webuye," Ng’etich alisema Jumanne.

Ng'etich alisema baada ya ukaguzi wa kitaalamu kutoka kwa Idara ya Makosa ya Jinai (DCI) ilibainika kuwa thamani ya bangi hiyo ilikadiriwa kuwa Sh15M. 

Aliwapongeza wananchi kwa kuripoti uhalifu huo. Ng'etich alishukuru uhusiano mzuri kati ya polisi na wananchi akiwataka kuwa macho na kuripoti kesi kama hizo. 

Aliwaonya madereva dhidi ya kujihusisha na usafirishaji wa bangi na vitu vingine kinyume na sheria. 

Hata hivyo, aliwataka askari wa trafiki kuwa makini, kuwatambua madereva watukutu na kuwakamata ili kuwa mfano kwa wengine.

Kosa la ulanguzi wa bangi nchini Kenya linaweza kualika adhabu ya hadi miaka 50 gerezani au faini ya hadi Milioni 50.