Hofu baada ya walinzi wawili wauawa kinyama na majambazi Machakos

Muhtasari

•Kamanda wa polisi wa Kangundo Edward Changach amesema wawili hao waliuawa na genge moja katika matukio  tofauti  asubuhi ya Jumatano.

•Polisi wameanzisha uchunguzi kubaini sababu ya mauaji ya walinzi wasio na hatia waliokuwa wakirejea nyumbani. 

Umma wazingira eneo ambapo mlinzi wa usiku alipatikana ameuawa katika soko la Kivaani huko Kangundo, Kaunti ya Machakos Jumatano.
Umma wazingira eneo ambapo mlinzi wa usiku alipatikana ameuawa katika soko la Kivaani huko Kangundo, Kaunti ya Machakos Jumatano.
Image: GEORGE OWITI

Walinzi wawili wameuawa na watu wanaoshukiwa kuwa majambazi katika eneo la Kangundo, Kaunti ya Machakos. 

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Kangundo Edward Changach amesema wawili hao waliuawa na genge moja katika matukio  tofauti  asubuhi ya Jumatano.

"Leo asubuhi ndani ya kaunti ndogo ya Kangundo, tumeamka na kugundua kuwa tulikuwa na visa viwili vya mauaji katika kaunti ndogo," Changach alisema.

Changach alisema tukio la kwanza lilitokea katika soko la Kivaani mwendo wa saa sita usiku, huku la pili likitokea katika soko la Katanga.

"Moja ilitokea katika soko la Kivaani ambapo kulikuwa na mlinzi ambaye alikuwa akirejea nyumbani usiku wa manane. Alizuiliwa na genge lisilojulikana na akauawa," Changach alisema.

Mkuu wa polisi alisema silaha ya mauaji,  kifaa chenye ncha kali kilipatikana katika eneo la tukio.

 "Mwendo wa saa kumi na moja asubuhi, genge hilo hilo ndani ya soko la Katanga lilimvizia mlinzi mwingine ambaye alikuwa akitokea zamu katika kitongoji cha Kangundo na wakamkatakata kwa kitu chenye ncha kali. Alikufa papo hapo," Changach alisema.

 Changach alisema polisi wameanzisha uchunguzi kubaini sababu ya mauaji ya walinzi wasio na hatia waliokuwa wakirejea nyumbani. Alisema wameanzisha  msako mkali dhidi ya washambuliaji hao. Changach alisema matukio hayo yalikuwa ya pekee katika kaunti ndogo ya Kangundo.

"Hatujawahi kuwa na matukio kama haya katika siku za hivi karibuni. Lakini, pia ni wito wangu kwa wananchi ambao wanaweza kuwa na taarifa za kushiriki na polisi ili tuwakamate washukiwa," Changach alisema.