IG Japhet Koome azungumzia madai ya kuondolewa kwa walinzi wa Mama Ngina

Koome alikanusha madai kwamba walinzi wa Mke wa Rais wa zamani wameitwa.

Muhtasari

•IG alisema Huduma ya Kitaifa ya Polisi inaendelea kuhakikisha kuwa Wake wa Marais wa zamani akiwemo Mama Ngina, wako wazima na salama.

•Koome alisema anawaheshimu wazee ambao wametumikia nchi na atahakikisha wako salama 'huku wakifurahia kustaafu'.

akiwahutubia wanahabari katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi mjini Mombasa katika picha hii iliyopigwa tarehe 3 Feb 2023.
Inspekta jenerali wa Polisi Japheth Koome akiwahutubia wanahabari katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi mjini Mombasa katika picha hii iliyopigwa tarehe 3 Feb 2023.
Image: Laban Walloga

Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome amethibitisha kuwa hakujawa na mabadiliko yoyote katika ulinzi wa mke wa rais wa zamani Jomo Kenyatta, Mama Ngina.

IG alisema Huduma ya Kitaifa ya Polisi inaendelea kuhakikisha kuwa Wake wa Marais wa zamani akiwemo Mama Ngina, wako wazima na salama.

Koome alikanusha madai kwamba walinzi wa Mke wa Rais wa zamani wameitwa, akisema hataingizwa kwenye 'mazungumzo ya kisiasa.'

"Mke wa rais wa zamani ana usalama, tunalinda majengo yake, na sio yeye peke yake. Tunatoa usalama kwa sababu tunaheshimu afisi hizo,” Koome aliambia vyombo vya habari Ijumaa.

Kumekuwa na madai kuwa usalama wa Mama Ngina ulikuwa umeathiriwa huku kukiwa na madai kwenye mitandao ya kijamii kwamba aliachwa Mombasa na walinzi wake walioitwa.

Siku ya Ijumaa, Koome alisema anawaheshimu wazee ambao wametumikia nchi na atahakikisha wako salama 'huku wakifurahia kustaafu'.

"Mke wa rais wa zamani ana usalama, huo ndio msimamo, tusikisie," Koome alisema.

Mama Ngina ni mke wa Rais mwanzilishi Jomo Kenyatta ambaye alifariki dunia mwaka wa 1978.