Jamaa akamatwa kwa madai ya kulawiti mvulana wa miaka 4 na kumkata sehemu za siri

Kijana wa miaka 18 amedaiwa kulawiti mvulana wa miaka 4 kisha kumkata sehemu zake za siri.

Muhtasari

•Inadaiwa mvulana huyo alifungiwa ndani ya nyumba katika Soko la Ikombe kabla ya mshukiwa anayesemekana kuwa na ugonjwa wa akili kufanya kitendo hicho cha kinyama.

•Mwathiriwa alikimbizwa katika kituo cha afya cha eneo hilo ambako alipata huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa katika hospitali ya Matuu Level Four.

Crime Scene
Image: HISANI

Polisi katika kaunti ya Machakos wanamzuilia kijana wa miaka 18 anayedaiwa kulawiti mvulana wa miaka 4 kabla ya kumkata sehemu zake za siri.

Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Yatta Jane Makau alithibitisha kisa hicho akisema mvulana huyo alifungiwa ndani ya nyumba katika Soko la Ikombe kabla ya mshukiwa anayesemekana kuwa na ugonjwa wa akili kufanya kitendo hicho cha kinyama.

Mwathiriwa alikimbizwa katika kituo cha afya cha eneo hilo ambako alipata huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa katika hospitali ya Matuu Level Four.

"Mtoto huyo alipokea huduma ya kwanza katika zahanati ya kibinafsi na baadaye akakimbizwa katika Hospitali ya Matuu Level Four. Baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi kwa matibabu zaidi," polisi walisema.

Mtuhumiwa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Ikombe akisubiri kusomewa mashtaka yake.

Kwingineko, Mwanamke mmoja ameingia mitini baada ya kudaiwa kumdunga kisu na kumuua mpenzi wake katika mtaa wa Bahati, jijini Nairobi.

James Mungai Wirura alipatikana akiwa na maumivu ndani ya nyumba yake baada ya kudungwa kisu kifuani.

Alikimbizwa katika hospitali ambapo alitangazwa kufariki. 

Polisi na mashahidi wanasema marehemu aligombana na mpenzi wake aliyetambulika kwa jina la Everline kabla ya ugomvi huo kuwa vita.

Mwanamke huyo alichukua kisu kutoka jikoni, akamchoma mpenziwe na kutoroka eneo hilo.

Mkuu wa polisi wa Nairobi James Mugera alisema wanachunguza tukio hilo na wanamsaka mshukiwa anayejulikana kujibu mashtaka kuhusiana na mauaji hayo.