Jinsi jambazi aliyeuawa Samuel Muvota alivyotumia warembo zaidi ya 50 kuwaibia wanaume

Muhtasari

•Baada ya kuwaajiri wanawake hao Muvota angewatuma katika miji mikubwa tofauti nchini ili wamsaidie kuiba kutoka kwa watu wanaotembelea maeneo ya burudani.

•Wanawake hao walitumia dawa inayopatiwa wagonjwa wenye matatizo ya kiakili katika Hospitali ya Mathare ili kuwafanya wahasiriwa wao wapoteze fahamu.

•Kuna baadhi ya wanaume ambao wangepatikana uchi kwenye magari yao wakiwa wamevalia kondomu.

Marehemu Samuel Mugo Muvota
Marehemu Samuel Mugo Muvota
Image: TWITTER// DCI

Wapelelezi wa DCI wameendelea kufichua maisha ya giza ya mwanaume aliyeuawa Jumatatu kwa kupigwa risasi mchana peupe katika eneo la Mirema, Kasarani.

Uchanganuzi wa hifadhi data umebaini kuwa Samuel Mugoh Muvota amekuwa akiishi maisha ya uhalifu tangu mwaka wa 2011.

Kufuatia taarifa ya awali ya DCI kuwa Muvota aliajiri zaidi ya  wanawake 50 warembo na wenye sura za kupendeza, kitengo hicho kimetoa maelezo zaidi kuhusu jinsi marehemu alivyowatumia wanadada hao kutekeleza uhalifu wake.

Baada ya kuwaajiri wanawake hao Muvota angewatuma katika miji mikubwa tofauti nchini ili wamsaidie kuiba kutoka kwa watu wanaotembelea maeneo ya burudani.

"Jijini Nairobi, walitembelea kilabu cha Switch cha Kasarani, Whisky River kando ya barabara ya Kiambu, Red Lion mjini Ruaka, Oklahoma Choma Zone, Lacascada, Aroma, Backroom, Mkwanju, Dragon na vilabu vyote vilivyo kando ya barabara ya Kamiti kutoka Roysambu, 44 na Zimmerman," Kitengo cha DCI kimefichua.

Walipowasili kwenye vilabu hivyo wanawake hao waliagiza vileo ghali ili kuepuka kutuhumiwa kuwa watu na kuwavutia wanaume walio karibu kuungana nao. Muvota angelipa bili yote kutoka nyumbani kwake Roysambu  ama Githurai.

Aghalabu wanawake hao walitumia dawa inayopatiwa wagonjwa wenye matatizo ya kiakili katika Hospitali ya Mathare ili kuwafanya wahasiriwa wao wapoteze fahamu.

Wangewaeka dawa hiyo m'aarufu kama 'mchele' kwenye kinywaji cha mhasiriwa wao kulingana na kinga yao.

Ikiwa mhasiriwa alionekana kuwa mwangalifu na kinywaji walichotia dawa, wanawake hao badala yake wangempa kinywaji cha kuongeza nguvu wakidai kuwa kingesaidia kwa shughuli ya kitandani ambayo ingeendelea baada ya wao kuondoka pale. Wangeendelea kumtongoza mhasiriwa wakisubiri apoteze fahamu ili waweze kumwibia.

Ujanja huo ukikosa kufua dafu wanawake hao wangeandamana na wahasiriwa hadi nyumbani kwao kisha kujitolea kupika. Wangetumia fursa hiyo kumtilia dawa mhasiriwa kisha kutoroka na baadhi ya mali yao.

Cha kushangaza ni kuwa hakuna mhasiriwa yeyote wa genge la Muvota anayekumbuka akishiriki mapenzi na wanawake hao. Kuna baadhi yao ambao wangepatikana uchi kwenye magari yao wakiwa wamevaa kondomu ila imebainika huo ulikuwa ujanja tu wa kuwafanya wahasiriwa wasitafute usaidizi mara moja baada ya kurejesha fahamu.

Muvota alihakikisha wanawake ambao aliajiri waliishi katika mtaa mmoja ambapo angewatembelea virahisi na kuchukua mali ambayo walikuwa wamekusanya kutoka kwa wahasiriwa wao.  Baada ya hapo angewalipa donge nono.

Marehemu alimiki akaunti za benki zaidi ya 300 ambazo alitumia kuweka pesa zilizotokana na uhalifu. Alimiki magari zaidi ya sita ambayo alitumia kusafiri kutoka eneo moja hadi nyingine.

Muvota alikuwa amefikishwa mahakamani mara kadhaa kabla ya mauaji yake ila kila mara akaweza kukwepa kifungo kwa njia za kushangaza.