Jinsi tapeli alivyowaibia wanunuzi kwa kuwauzia mchanga kwenye pakiti za unga wa ngano

Mlalamishi alipigwa na butwaa alipogundua kuwa pakiti za unga kwenye mifuko saba aliyonunua zilikuwa zimejazwa na mchanga.

Muhtasari

•Bi Fatuma Issa na msaidizi wake Tony Molaya walikamatwa Jumamosi ndani ya eneo la Adere baada ya uchunguzi kuwaelekeza maafisa wa polisi kwao.

•Polisi wamesema jumla ya pakiti 240 za mchanga uliodaiwa kuwa unga na marobota matatu zilipatikana wakati wa operesheni hiyo.

Image: NPS

Polisi katika kaunti ya Tana River wanawashikilia washukiwa wawili kwa madai ya kuwauzia wateja mchanga uliopakiwa kwenye pakiti za unga wa ngano.

Mfanyabiashara Bi Fatuma Issa na msaidizi wake Tony Molaya walikamatwa siku ya Jumamosi ndani ya eneo la Adere baada ya uchunguzi kuwaelekeza maafisa wa polisi kwao.

Kulingana na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), maafisa walikuwa wameanzisha uchunguzi wa kina kufuatia malalamishi kutoka kwa muuzaji rejareja katika Kituo cha Biashara cha Madogo ambaye alikuwa amenunua mifuko saba ya ‘Unga wa Ngano wa Ajab’ kutoka kwa mshukiwa kwa gharama ya Ksh 11,900.

Mlalamishi alikumbwa na mshtuko mkubwa alipofika kwenye duka lake na kugundua kuwa pakiti za unga kwenye mifuko saba aliyonunua zilikuwa zimejazwa na mchanga na wala si unga wa ngano kama ilivyodaiwa.

"Mshukiwa amekamatwa pamoja na msaidizi wake, Tony Molaya, 38, katika eneo la Adere, walipokuwa katika harakati za kujaza mchanga kwenye pakiti na marobota ya Ajab," NPS imesema.

Polisi wameripoti kuwa jumla ya pakiti 240 za mchanga uliodaiwa kuwa unga na marobota matatu zilipatikana wakati wa operesheni hiyo.

"Walalamishi wengine wawili tangu wakati huo wametoa ripoti zaidi za kununua mchanga katika marobota yenye chapa ya Ajab," polisi walisema.

Washukiwa hao wawili kwa sasa wako chini ya ulinzi wa polisi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo huku uchunguzi ukiendelea.