Mahakama yaagiza IEBC kumuidhinisha Karungo Thang'wa kuwania useneta Kiambu

Mahakama iliamuru IEBC kuweka jina la Thang'wa kwenye karatasi za kura

Muhtasari

•Mahakama alifuta uamuzi wa IEBC kwa misingi ya kukosa ushahidi wa kutosha kupelekea Thang'wa kuondolewa madarakani.

•Mahakama iliamuru IEBC kuweka jina la Thang'wa kwenye karatasi za kura na kumpatia kibali cha kuwania.

katika mkutano wa kisiasa wa UDA
Naibu Rais William Ruto na mgombea useneta wa Kiambu Karungo Thang'wa katika mkutano wa kisiasa wa UDA
Image: FACEBOOK// KARUNGO THANG'WA

Mahakama kuu imefupilia mbali uamuzi wa IEBC la kumzuia Karungo Thang'wa kuwania useneta wa kaunti ya Kiambu.

IEBC ilikuwa imemzuia mgombea huyo kwa tiketi ya UDA kwa misingi kung'atuliwa kutoka kwa ofisi ya umma kwa madai ya ulaghai.

Alhamisi jaji Rachael Ng'etich alifuta uamuzi wa IEBC kwa misingi ya kukosa ushahidi wa kutosha kupelekea Thang'wa kuondolewa madarakani kama CEC katika kaunti ya Kiambu.

"Mahakama hii inakosa sababu ya kumzuia Karungo Thang'wa kuwania useneta wa Kiambu," Mahakama Kuu iliamuru.

Mahakama hiyo iliamuru IEBC kuweka jina la Thang'wa kwenye karatasi za kura na kumpatia kibali cha kuwania.

Akisherehekea uamuzi huo wa mahakama, Thang'wa alimshukuru Mola na wakazi wa Kiambu kwa kusimama naye.

"Mungu wetu ni Mungu wa nafasi nyingine. Mahakama kuu imeamuruIEBC kunipa kibali mara moja! Mahakama pia imesema kwamba sikuwahi kung'atuliwa mamlakani, lakini niliondoka madarakani kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 179(7) cha katiba. Asante wakazi wa Kiambu kwa maombi na Msaada wako Tuko Kwa Debe!" Thang'wa aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Mgombea useneta huyo alielekea mahakamani mwezi jana baada ya IEBC kukosa kumuidhinisha kuwania wadhifa huo.

Aliwahi kuwania kiti hicho katika uchaguzi wa 2017 ila akapoteza kwa seneta wa sasa Kimani Wamatangi.