Mshtuko baada ya mama kuwaua wanawe 3 kabla ya kujaribu kujitoa uhai bila mafanikio Kiambu

Mshukiwa alikuwa ameandika barua kabla ya kujaribu kujitoa uhai.

Muhtasari

•Mwanamke huyo anaripotiwa kuwaua watoto hao wa miaka minne, miaka mitatu na mdogo wa miezi 6 ndani ya nyumba yao ya kupanga.

•"Ni kama alitoka juu ya sink akanguka chini. Tayari alikuwa amejikatakata kwa kisu mwili mzima," jirani alisimulia

Crime scene
Crime scene
Image: MAKTABA

Hali ya mshtuko na huzuni ilitanda katika eneo la Thogoto, kaunti ndogo ya Kikuyu wikendi baada ya mwanamke mmoja mwenye umri wa makamo kudaiwa kuwaua watoto wake watatu wadogo kabla ya kujaribu kujitoa uhai.

Mwanamke huyo anaripotiwa kuwaua watoto hao wa miaka minne, miaka mitatu na mdogo wa miezi 6 ndani ya nyumba yao ya kupanga.

Shahidi mmoja aliambia Kameme TV kwamba majirani walikimbia  katika eneo la uhalifu baada ya kusikia kishindo kikubwa kutoka kwa nyumba hiyo. majirani walipoingia ndani ya nyumba ya mshukiwa walikuta mwanamke huyo akiwa amelala kwenye sakafu huku miili ya watoto wake ikiwa imelazwa juu ya kitanda kimoja.

"Tulipata ni kama mama alikuwa anajaribu kujitia kitanzi. Ni kama alitoka juu ya sink akanguka chini. Tayari alikuwa amejikatakata kwa kisu mwili mzima," jirani mmoja alisimulia.

Aliongeza, "Hatukuona ata mtoto mmoja. Hapo ndipo nilipoingia ndani ya chumba cha kulala. Kuingia nilipata watoto wamelazwa hapo kama migomba."

Bosi wa polisi katika eneo la Kikuyu, Bw Ronald Kirui, alisema mwanamke huyo tayari ametiwa mbaroni na atafikishwa mahakamani Jumatatu. Mumewe ambaye hakuwa nyumbani wakati wa tukio hilo pia alikamatwa ili kusaidia katika uchunguzi.

"Kwa sasa hatuwezi kubaini sababu ambayo ilipelekea kifo cha watoto hawa watatu. Tumeanzisha uchunguzi. Mama alitaka kujitoa uhai lakini kwa bahati nzuri majirani walisaidia kuzuia," Bw Kirui alisema.

Kirui alidokeza kwamba mzozo wa kifamilia wa muda mrefu huenda ulichangia katika mauaji hayo ya kinyama.

Aidha, alifichua kuwa mshukiwa alikuwa ameandika barua kabla ya kujaribu kujitoa uhai. Barua hiyo itasaidia katika uchunguzi.

Mili ya watoto hao wadogo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia miili huku uchunguzi wa maiti ukipangwa kufanyika.