Mvulana amuua binamuye kwa mkuki baada ya kuzozana kuhusu nani angechaji simu kwanza

Mshukiwa alitoweka punde baada ya kutekeleza unyama huo.

Muhtasari

•Mshukiwa anaripotiwa kumdunga Josphat Kibet ,31, kwa mkuki Jumapili jioni wakiwa nyumbani kwao katika eneo la Kaimosi.

•Mshukiwa alitoweka punde baada ya kutekeleza unyama huo huku Kibet akichukuliwa na kukimbizwa hospitalini.

Crime scene
Crime scene
Image: MAKTABA

Polisi katika kaunti ya Nandi wanamsaka mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 17 kwa madai ya kumuua binamu yake.

Mshukiwa anaripotiwa kumdunga Josphat Kibet ,31, kwa mkuki Jumapili jioni wakiwa nyumbani kwao katika eneo la Kaimosi.

Wanafamilia hao wawili wanadaiwa kuzozana kuhusu nani angechaji simu yake wa kwanza kabla ya mshukiwa kuchukua mkuki na kumdunga Kibet kwenye upande wa kushoto wa kifua chake.

Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa mshukiwa alitoweka punde baada ya kutekeleza unyama huo huku Kibet akichukuliwa na kukimbizwa katika hospitali ya Kapsabet County Referral.

"Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa wawili hao walibishana kuhusu nani angechaji simu yao kwanza, kabla ya kijana huyo kufikia mshale, akamchoma marehemu upande wa kushoto wa kifua chake kabla ya kuondoka," Taarifa iliyochapishwa na DCI Jumatatu asubuhi imesema.

Kwa bahati mbaya mhasiriwa tayari alikuwa amepoteza maisha yake kabla ya kufikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Polisi wameanzisha msako mkali wa kumtafuta mshukiwa ambaye kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya mauaji.