Mwanajeshi taabani kwa kumfyatulia risasi mwanabodaboda aliyemfikisha bintiye nyumbani usiku

Inadaiwa kuwa daktari huyo wa kijeshi huenda alimshuku Atendo kuwa mpenzi wa bintiye.

Muhtasari

•Wycliffe Atendo alinusurika kifo baada ya baba huyo wa mwanadada ambaye alikuwa amebeba kumshambulia kwa risasi.

•Mwanadada huyo alipofikishwa nyumbani babake alitokea kwenye lango huku akiwa amejawa na hasira na kumpiga vibaya kabla ya kumwelekeza aingie ndani.

DCI yafichua jinsi bunduki ya polisi ilivyosababisha ugaidi Nairobi kwa miaka 3
Image: DCI/TWITTER

Daktari wa kijeshi anazuiliwa katika kituo kimoja cha jeshi jijini Nairobi baada ya kudaiwa kufyatua risasi kuelekeza kwa mwendesha bodaboda aliyemdondosha binti yake nyumbani  Alhamisi jioni.

Kitengo cha DCI kimeripoti kwamba Wycliffe Atendo alinusurika kifo baada ya baba huyo wa mwanadada ambaye alikuwa amebeba kumshambulia kwa risasi. Inadaiwa kuwa daktari huyo wa kijeshi huenda alimshuku Atendo kuwa mpenzi wa bintiye.

Mhasiriwa alimchukua mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 21 nje ya duka moja la dawa katika Kimathi Street, Nairobi na kumpeleka nyumbani kwao katika eneo la Syokimau, kaunti ya Machakos ambako ni safari ya takriban kilomita 20.

Wakati mwanadada huyo alipokuwa anamlipa mhudumu huyo wa bodaboda, babake ambaye ni daktari wa kijeshi alitokea kwenye lango huku akiwa amejawa na hasira na kumpiga vibaya kabla ya kumwelekeza aingie ndani.

"Mwendesha nduthi huyo alipokuwa akitafakari hatua ya kuchukua, mwanamume huyo mwenye hasira alitoa bunduki yake na kumfyatulia risasi, na kumfanya atoroke eneo la tukio ili kuokoa maisha yake," Kitengo cha DCI kimesema kupitia taarifa.

Baada ya tukio hilo la kushtua, mwendesha bodaboda huyo alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Syokimau na maafisa kadhaa wakapiga hatua ya kuelekea nyumbani kwa mshukiwa ili kuthibitisha madai hayo.

Dakatari huyo wa kijeshi alitiwa pingu na bastola yenye risasi 42 kupatikana katika makazi hayo yake.

Mshukiwa alipelekwa hadi kituo cha kijeshi ambapo anazuiliwa huku akingoja kuadhibiwa kwa kutumia sheria za kijeshi.