Rais Uhuru Kenyatta azindua rasmi barabara ya Nairobi Expressway

Uzinduzi rasmi unamaanisha kuwa barabara hiyo itapatikana tena kwa matumizi ya umma

Muhtasari

•Barabara ya Expressway ilikuwa imefungwa Jumamosi mwendo wa saa tatu usiku kufuatia kupita kwa kipindi cha majaribio

•Rais Kenyatta  pia ameizindua rasmi barabara ya Nairobi Eastern Bypass  yenye  urefu wa kilomita 27.8.

Rais Kenyatta akizindua barabara ya Eastern Bypass mnamo Julai 31, 2022
Rais Kenyatta akizindua barabara ya Eastern Bypass mnamo Julai 31, 2022
Image: IKULU YA KENYA

Rais Uhuru Kenyatta amezindua rasmi barabara kuu ya Nairobi Expressway.

Barabara ya Expressway ilikuwa imefungwa Jumamosi mwendo wa saa tatu usiku kufuatia kupita kwa kipindi cha majaribio.

Uzinduzi rasmi sasa unamaanisha kuwa barabara hiyo itapatikana tena kwa matumizi ya umma

Kampuni ya Moja Expressway ambayo inasimamia barabara hiyo ilitangaza kuwa itatumika tena pindi itakapozinduliwa rasmi.

Akizindua mradi huo, Uhuru alisema mradi huo ni marekebisho ya kimsingi ya jinsi serikali inaweza kutumia muundo wa PPP ili kupunguza upungufu wa miundombinu.

"Hongera kwa wote waliofanikisha kazi hii bora na kwa serikali na watu wa Kenya kwa kuwa na imani na miradi yetu ya miundombinu," alisema.

“Shukrani zetu ziende kwa CRBC kwa kuchagua kuwekeza na kuonyesha imani yao kwa nchi yetu.

Rais Kenyatta  pia ameizindua rasmi barabara ya Nairobi Eastern Bypass  yenye  urefu wa kilomita 27.8.

Barabara hiyo ilipanuliwa kutoka kuwa ya  njia mbili hadi kuwa barabara ya njia nne, mradi ambao uligharimu Ksh 12.5B.

Inaunganisha barabara mbili kuu za Mombasa Road na Thika Super Highway.

"Ilipanuliwa kama sehemu ya juhudi endelevu za serikali kupunguza msongamano Nairobi," Taarifa ya Ikulu ya Kenya imesema.