(+Video) Jamaa asakwa kwa madai ya kupanda bangi ya thamani ya 1M ndani ya nyumba yake

Bangi hiyo ilikuwa imepandwa kwenye chumba cha kulala, cha maakuli na sebuleni.

Muhtasari

•Mimea 21 ya bangi ilipatikana kwenye chumba cha kulala, mingine 68 ikapatikana sebuleni na 14 kwenye chumba cha maakuli.

•Bangi hiyo ilipimwa na kufikia kilo 33.5 na inakadiriwa kuwa na thamani ya takriban shilingi milioni moja.

iliyopatikana katika nyumba moja mjini Eldoret.
Mimea ya bangi iliyopatikana katika nyumba moja mjini Eldoret.
Image: NPS

Polisi katika kaunti ya Uasin Gishu wanamsaka jamaa mmoja anayetuhumiwa kupanda mimea ya bangi ndani ya nyumba ya kupanga.

Msako dhidi ya Michael Kibet ulianzishwa baada ya mimea 129 ya bangi kupatikana ndani ya nyumba iliyo katika mtaa wa Elgon View, jijini Eldoret.

Polisi wameripoti kuwa mimea 21 ilipatikana kwenye chumba cha kulala, mingine 68 ikapatikana sebuleni na 14 kwenye chumba cha kulia.

Mimea mingine 26  ya bangi pia ilipatikana ndani ya nyumba ya mabati  iliyokuwa karibu na nyumba kuu.

"Mimea yote iling'olewa baada ya maafisa wa DCI  kuandika taarifa ya eneo la uhalifu," Taarifa iliyotolewa Jumatano na tume ya huduma kwa polisi ilisoma.

Bangi hiyo ilipimwa na kufikia kilo 33.5 na inakadiriwa kuwa na thamani ya takriban shilingi milioni moja.

"Tunatoa wito kwa taarifa zozote zinazoweza kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa na kuwataka wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu," Taarifa ya polisi ilisoma.

Haya yanajiri huku kukiwa na mjadala mkubwa unaoendelea kuhusu uhalalishaji wa ukulima wa bangi ambao kwa sasa umeharamishwa hapa nchini.

Hii ni baada ya mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi wa mwaka huu kupendekeza ukulima wa mmea huo ambao kwa sasa ni haramu.

Profesa George Wajackoyah wa Roots Party ameahidi kuhalalisha ukulima wa bangi na matumizi yake kwa minajili ya matibabu iwapo atachaguliwa kuwa rais.

Mwezi jana mgombea urais huyo alisema anatazamia kufanya maeneo ya  Bunyore, Mlima Kenya, Nyamira na Kisii kuwa maeneo makuu ya kilimo cha mmea huo ambao kwa sasa ni haramu hapa nchini.

"Bunyore katika mkoa wa Nyanza kuna mojawapo ya hali bora ya anga  ya kukuza bangi kwa sababu inakua kiasili. Nyamira Kisii na eneo la Mlima Kenya zitakuwa kipaumbele chetu kwa sababu tunataku kuinua Bunyore kuwa kaunti na huenda tutakuwa tunaagiza wakazi wa Bunyore kuwa na  bangi zao kuu," Alisema Wajackoyah.

Akiwa kwenye mahojiano ya awali Wajackoyah alidai kuwa Wakenya wataruhusiwa kulima bangi kwa ajili ya kuuza nje, hatua ambayo anasema itaongeza mzunguko wa pesa katika uchumi huku akidai kuwa gunia moja linaweza kuuzwa kwa dola milioni 3.2.