Wakenya wamekopa bilioni 1.4 kutoka kwa Hustler Fund - Serikali

Waziri Simon Chelugui alisema wateja 5,191,542 wamejisajili kupata huduma za Hustler Fund.

Muhtasari

•Jumla ya mikopo ambayo imechukuliwa ni 2,346,675 huku Sh48,526,204 tayari zikiwa zimerejeshwa.

•Hazina hiyo imeundwa mahususi kusaidia wafanyabiashara wadogo nchini.

Image: HISANI

Jumla ya Sh1,381,747,777 za Hustler Fund zilikuwa zimetolewa kwa Wakenya kufikia Ijumaa usiku wa manane.

Katika taarifa yake ya Jumamosi, Waziri wa Vyama vya Ushirika na MSMEs Simon Chelugui alisema kuwa wateja 5,191,542 wamejisajili kupata huduma za Hustler Fund.

Jumla ya mikopo ambayo imechukuliwa ni 2,346,675 huku Sh48,526,204 tayari zikiwa zimerejeshwa.

Takwimu zilizotolewa na serikali zinaonyesha kuwa kila sekunde Wakenya wanafanya takriban miamala 223 ya mikopo ya hazina hiyo.

Hazina hiyo imeundwa mahususi kusaidia wafanyabiashara wadogo nchini.

Rais William Ruto alizindua hazina hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu siku ya Jumatano akitimiza ahadi yake ya kabla ya uchaguzi ya kutenga Sh50 bilioni kwa ajili ya 'mahustlers.'

"Kupitia uzinduzi wa hazina hii, tunasaidia Wakenya wasio na uwezo wa kutosha kwa huduma na bidhaa zinazoitikia biashara zao na vile vile kuwakomboa kutoka kwa mawakala na kuanzisha utamaduni wa kuweka akiba, uwekezaji na usalama wa kijamii," Ruto alisema.

Hustler Fund inaundwa na bidhaa nne – za kibinafsi, biashara ndogo, SME na mikopo ya kuanzia.

Ili kupata hazina hiyo, Wakenya wanaweza kubonyeza *254# kwenye simu zao za rununu.