Wanabodaboda 16 wanaotuhumiwa kunyanyasa dereva mwanamke kuzuiliwa siku 15

Washukiwa hao hawakuwakilishwa na wakili yeyote.

Muhtasari

•Hakimu Robert Shikwe wa mahakama ya Milimani alikubali ombi la upande wa mashtaka la kuzuilia washukiwa hao ili kukamilisha uchunguzi.

•Mhasiriwa alipokuwa ndani ya gari lake washukiwa walianza kumyanyasa na katika harakati hizo wakamnyang’anya simu yenye thamani ya Sh130,000.

Baadhi ya waendesha bodaboda 16 waliofikishwa mbele ya Mahakama ya Milimani Jumatano walishtakiwa kwa kumnyanyasa kingono mwanamke dereva katika Barabara ya Wangari Maathai, Machi 9, 2022.
Baadhi ya waendesha bodaboda 16 waliofikishwa mbele ya Mahakama ya Milimani Jumatano walishtakiwa kwa kumnyanyasa kingono mwanamke dereva katika Barabara ya Wangari Maathai, Machi 9, 2022.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Waendesha bodaboda 16 ambao wanatuhumiwa kunyanyasa dereva wa kike katika barabara ya Wangari Maathai watazuiliwa kwa siku 16 zaidi.

Hakimu Robert Shikwe wa mahakama ya Milimani alikubali ombi la upande wa mashtaka la kuzuilia washukiwa hao ili kukamilisha uchunguzi.

Alisema suala hilo ni la maslahi ya umma, na ipo haja ya polisi kupewa muda wa kuwachunguza washukiwa hao.

Kesi  hiyo itatajwa tena Machi 24.

Mnamo Jumatatu, polisi waliwasilisha ombi la kutaka kuwazuilia washukiwa James Mutinda, Samuel Wafula, Charles Omondi, Japheth Bosire, Hassan Farah, Wanjiku Lincon, Harrison Maina, miongoni mwa wengine.

Inspekta Yvonne Mwanzia alisema washukiwa hao walimshambulia mwanamke huyo ambaye ni mwanadiplomasia  mnamo Machi 4 kwenye barabara ya Wangari Maathai jijini Nairobi.

Afisa huyo aliomba polisi kuruhusiwa kuwazuilia washukiwa hao kwa siku 20 ili waweze  kukamilisha uchunguzi wao.

Washukiwa hao hawakuwakilishwa na wakili yeyote.

Mwanzia aliambia mahakama kuwa mhasiriwa alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Parklands Ijumaa jioni baada ya kuvamiwa na kikundi cha wanabodaboda.

Alisema mwendo wa  saa kumi na moja unusu jioni ya Machi 4, mwathiriwa alipokuwa akiendesha gari lake kwenye barabara ya Wangari Mathai alihusika kwenye ajali na mwendesha bodaboda alipofika Barabara Tano,

"Ghafla kundi la waendesha bodaboda walikimbia mahali ambapo gari lake lilikuwa limesimama na kumvamia huku wakimshtumu kwa kumgonga mmoja wao," mahakama iliambiwa.

Afisa huyo aliongeza kuwa mhasiriwa alipokuwa ndani ya gari lake washukiwa walianza kumyanyasa na katika harakati hizo wakamnyang’anya simu yenye thamani ya Sh130,000.

Polisi wanahitaji kupata picha za CCTV kutoka Barabara Tano kwa uchunguzi wa kitaalamu katika idara ya upigaji picha  ya DCI.

Pia wanahitaji muda wa kutayarisha faili na kulipeleka kwa DPP.

Alisema kuwa mhasiriwa anaendelea kupokea matibabu na ushauri wa kitaalumu kutoka kwa mwanasaikolojia.

 Baadhi ya washukiwa walipinga siku 20 ambazo polisi waliomba. Walikana madai ya polisi kuwa wao ni waendesha bodaboda.