•Maafisa wa DCI wametoa wito kwa umma kusaidia katika kukamatwa tena kwa mshukiwa mkuu wa mauaji ya Kware.
•Wapelelezi wameomba watu kufichua habari kuhusu aliko mshukiwa kwa njia ya kisiri ya simu ya #FichuaKwaDCI.
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imetoa wito kwa umma kusaidia katika kukamatwa tena kwa mshukiwa mkuu wa mauaji ya Kware anayeripotiwa kutoroka kutoka kituo cha polisi..
Collins Jumaisi Khalusha anadaiwa kutoroka kutoka mikononi mwa polisi mnamo siku ya Jumanne, Agosti 20, pamoja na washukiwa wengine kumi na wawili. Alikuwa anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Gigiri na aliratibiwa kushtakiwa kwa mauaji.
Katika bango lililotolewa Alhamisi asubuhi, idara ya DCI ilitangaza kuwa zawadi ya pesa taslimu ambayo haijabainishwa itatolewa kwa yeyote ambaye atatoa habari zitakazosaidia kumkamata tena mshukiwa huyo anayetoka kaunti ya Vihiga.
"Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) inaomba usaidizi wa umma katika kutoa taarifa ambazo zinaweza kusaidia kukamatwa tena kwa Collins Jumaisi Khalusha. Alipangiwa kushtakiwa kwa mauaji lakini akatoroka kutoka mikononi mwa polisi mnamo Jumanne 19/8/2024,” bango lililotolewa na DCI lilisomeka.
Ilisomeka zaidi, "Zawadi kubwa ya pesa itatolewa kwa mtu yeyote aliye na habari za kuaminika zitakazopelekea mshukiwa kukamatwa. Mshukiwa anatoka lokesheni ndogo ya Shiru, lokesheni ya Shaviringa, Kaunti Ndogo ya Hamisi katika Kaunti ya Vihiga.”
Wapelelezi wameomba watu kufichua habari kuhusu aliko mshukiwa kwa njia ya kisiri ya simu ya #FichuaKwaDCI kwa nambari 0800722203 au nambari za 999, 911 na 112 za polisi.
Yeyote aliye na habari za kuaminika pia anaweza kuripoti katika kituo chochote cha polisi nchini, DCI imesema.
Collins Jumaisi ambaye ni mshukiwa mkuu wa mauaji ya makumi ya wanawake ambao miili yao ilipatikana katika eneo la kutupa taka la Kware, Nairobi aliripotiwa kutoroka katika kituo cha Polisi cha Gigiri mapema wiki hii..
Jumaisi alikuwa miongoni mwa washukiwa 13 waliotoroka kutoka kituo cha polisi. Wengine 12 waliotoroka kizuizini ni raia wa Eritrea.
Kisa hicho kilitokea Jumanne asubuhi. Polisi walifahamu hilo huku wakiwaamsha washukiwa wakiwa kizuizini kwa chai ya asubuhi.
Walikuwa wamekata matundu ya waya ambayo ni sehemu ya usalama kwa seli na kuinua ukuta wa mzunguko unaotoroka.