HAPANA! Wenye magari wapinga NTSA kuhusu ukaguzi wa magari ya kibinafsi

Muungano wa wenye magari nchini (KMA) umepinga vikali pendekezo la  maamlaka ya usalama barabarani NTSA  la kuanza ukaguzi wa magari yote ya kibinafsi . Kupitia taarifa kali yenye lalama nyingi kuhusu pendekezo hilo ,mwenyekiti wa muungano huo  Peter Murima amedai kwamba hatua hiyo imechochewa na uchu wa serikali kujipa mapato badala la usalama wa  magari hayo .Murima amesema tayari  wenye magari ya kibinafsi wanatozwa kodinzito na nyingi kwa kuyatumia magari yao ilhali  barabara kote nchini ni mbovu .

Maamlaka ya NTSA   wiki jana ilichapishwa  mswada wa mwongozo unaopendekeza na kutoa kanuni za jinsi magari yote yatakavyokaguliwa ili kudumisha usalama barabarani . Katika mapendekezo hayo ,NTSA itakuwa na maamlaka ya kuwapa   ruhusa wafanyibiashara wa kibinafsi kufungua vituo vya kuyakagua magari . Tayari NTSA imeanza kufanya vikao vya umma kuhusu  mapendekezo yake .

KMA imesema hatua hiyo ya serikali inalenga kuzidisha ufisadi ambao huambatana na zoezi zima la kuyakagua magari ya  usafiri wa umma nay ale ya kibiashara . Murima ,katika taarifa yake ameshangaa jinsi serikali ilivyokosa haya kwa kutaka kutwika mzigo zaidi wenye magari ilhali  tozo ya utunzi na ukarabati wa barabara imeongezwa kwa kutoska shilingi 8 hadi shilingi  24 ndani ya kipindi cha miaka miwili .Amesema  serikali kwanza inafaa kuziimarisha barabara zote nchini kabla ya kutekeleza   pendekezo la ukaguzi wa magari ya kibinafsi .