Harambee Starlets hawatoshiriki katika michuano ya Olimpiki 2020

Harambee Starlets hawatashiriki Olimpiki ya mwaka 2020 baada ya kubanduliwa nje ya raundi ya nne ya michuano ya kufuzu na Zambia kwa 1-0 na jumla ya mabao 3-2 ugani Nkoloma, Lusaka jana.

Starlets walihitaji ushindi ili kufuzu kwa raundi ya mwisho ya michuano hio ambapo wangechuana na aisha Ivory Coast au Cameroon.

Bodi ya uchaguzi ya FKF imetangaza vituo vya kaunti vya uchaguzi utakaoandaliwa katika kaunti 18 nchini. Uchaguzi huo utapelekea wajumbe kutoka kwa vilabu kwenye kaunti hizo kuwachagua wagombea 6 kwa kila tawi kuongoza ajenda yao ya kuendeleza soka.

Uchaguzi huo utafanyika wikendi ijayo. Bodi hio kwa sasa inathibitisha wapiga kura kufuatia kuchapishwa kwa orodha yao wiki iliyopita.

Bingwa wa mbio za Marathon Eliud Kipchoge yuko katika orodha ya mwisho ya wanariadha watano watakaotuzwa katika tuzo za wanariadha duniani huko Monaco.

Hata hivyo mwenzake Timothy Cheruiyot alibanduliwa nje ya orodha hiyo iliyotangazwa jana na IAAF. Wanariadha hao wengine ni mganda Joshua Cheptegei, Mwamerika Sam Kendricks, mwenzake Noah Lyles na raia wa Norway Karsten Warholm.

Unai Emery amepewa uungwaji mkono na usimamizi wa Arsenal lakini akaonywa kuwa lazima matokeo yaimarike. Kocha huyo mkuu amekua chini ya shinikizo kali kufuatia msururu wa matokeo mabaya na rekodi ya ushindi wa mechi mbili tu katika mechi kumi za ligi ya Primia.

Emery aliteuliwa kuchukua nafasi ya Arsene Wenger Mei mwaka wa 2018 na msimu wake wa kwanza uliishia na kushindwa mabao 4-1 na Chelsea katika fainali ya ligi ya Uropa.

Utumizi wa teknolojia ya VAR katika ligi ya Primia umepewa alama 7 kati ya 10 na wasimamizi wake licha ya kukashifiwa sana. Neil Swarbrick anasema VAR itaboreka na akawataka mashabiki kuwa na subira baada ya wiki nyingine ya utata.

VAR ilianza kutumika katika ligi ya Primia msimu huu baada ya kujaribiwa katika kombe la Carabao na FA, lakini imewakasirisha mashabiki wanaosema muda unaochukua kufanya maamuzi humaliza morali wa mechi.

Inaaminika kuwa usahihi wa maamuzi muhimu kama vile magoli, kadi nyekundu na penalti umeongezeka kutoka asilimia 82 msimu uliopita hadi asilimia 90 msimu huu.

Raheem Sterling hatacheza mechi ya Uingereza ya kufuzu kwa Uropa dhidi ya Montenegro Alhamisi kufuatia patashika lililozuka St George’s Park. Meneja wa Uingereza Gareth Southgate anasema Sterling alilumbana na Joe Gomez kufikia mwishoni mwa mechi ya Liverpool waliyoshinda 3-1 dhidi ya Man City jumapili. Inaarifiwa kuwa wawili hao walilumbana tena walipokutana jana kwa mazoezi ya Uingereza na kumpelekea Sterling kujiondoa kutoka kwa kikosi hicho.