Harambee Stars: Kimanzi amtema kipa Matasi, Shakava ajumuishwa

Kocha wa Harambee Stars Francis Kimanzi amemwondoa Patrick Matasi kutoka kwa kikosi chake cha wachezaji 23 kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Msumbiji itakayochezwa Oktoba tarehe 13 jijini Nairobi.

Kimanzi amewaweka wachezaji waliokua katika kikosi kilichotoka sare ya 1-1 na Uganda. Eric Johanna anayesakata soka Uswidi pia amewachwa nje huku Harun Shakava, Ian Otieno na Masud Juma wakijumuishwa.

Yusuf Mainge na Joseph Okumu pia wamejumuishwa. Timu hiyo itaripoti kambini Oktoba tarehe 7.

Hayo yakijiri, Kenya jana iliweza kupata medali moja tu katika fainali tatu za mbio zainazoendelea za ubingwa wa dunia huko Qatar.

Beatrice Chepkoech aliongoza kutoka mwanzo hadi mwisho wa mbio za mita elfu 3 kwa kinadada, kuruka viunzi na maji.  Juhudi za kupata medali katika mbio za wanaume za mita elfu 5 zitaendela leo baada ya Ethiopia kutamba katika fainali ya jana.

Jacob Kirop na Nicholas Kimeli walishindwa kuwapiku waEthiopia huku Muktar Edris akitetea taji lake na Selemen Barega akishinda nishani yafedha.

Hakukuwa na medali katika fainali ya mbio za kinadada za mita 800 kwani Eunice Sum alimaliza katika nafasi ya tano huku Mganda Halimah Nakaayi akishinda dhahabu.

Tukielekea kwenye kadanda, Ole Gunnar Solskjaer anasema Manchester United wana kibarua kigumu baada ya kutoka sare ya 1-1 na Arsenal.

Bao la kusawazisha la Pierre-Emerick Aubameyang lina maana kwamba United sasa hawajashinda mechi tatu za ligi msimu huu ambapo wamekua wakiongoza 1-0 kufikia muda wa mapumziko.

United wamekua na mwanzo mbaya wa ligi katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.

Manchester United wanatarajiwa kujaribu tena kumsajili mshambuliaji wa timu ya taifa ya Croatia na klabu ya Juventus Mario Mandzukic mwenye umri wa miaka 33, ambaye alikuwa kwenye mipango yao wakati wa dirisha la usajili lililopita.

Juve wanatarajiwa kutaka ada ya uhamisho ya pauni milioni 9, huku Mandzukic akitarajiwa kukataa ofa yoyote ya mshahara chini ya kiwango anacholipwa sasa cha pauni milioni 4.5 kwa mwaka.

Kiungo wa kati wa Wales Aaron Ramsey huenda akaanza katika mechi yake ya kwanza ya ligi ya mbaingwa kwa Juventus dhidi ya Bayer Leverkusen hii leo.

Ramsey, mwenye umri wa miaka 28, aliingia kama akiba katika mechi ya Juventus waliyotoka sare ya 2-2 dhidi ya Atletico Madrid mwezi September. Lakini ameanza mechi tatu za Serie A matches, ingawaje bado hajacheza kipindi cha dakika 90.