Harambee Stars na Togo watoka sare ugani Kasarani

Harambee-Stars
Harambee-Stars
Harambee Stars walitoka sare ya 1-1 jana na Togo katika mechi ya kufuzu kwa AFCON mwaka 2021 iliyochezwa uwanjani Kasarani.

Kiungo wa kati Johanna Omollo anayesakata soka Ubelgiji alifungia Stars kunako kipindi cha kwanza kabla ya Hakimu Oura-Sama kusawazishia Togo kunako dakika ya 64.

Matokeo haya yana maana kuwa vijana wa Francis Kimanzi hakuweza kupata ushindi waliohitaji kuwapandisha hadi kileleni mwa kundi G.

Uhispania walimaliza kampeni yao ya kufuzu kwa Uro mwaka 2020 kwa ushindi wa 5-0 dhidi ya Romania. Fabian Ruiz aliwapa mabingwa hao mara tatu wa Uropa uongozi wa mapema kabla ya Gerard Moreno kufunga kutoka kwa pasi ya Santi Cazorla.

Lionel Messi alifunga penalti ya dakika za lala salama, Argentina walipotoka sare ya 2-2 na Uruguay.  Mchezaji mwenza wa Barcelona Luis Suarez, alikua amewapa Uruguay uongozi kunako kipindi cha pili.

Nahodha huyo wa Argentina kisha akafunga bao lake la pili katika mechi za kimataifa. Edinson Cavani alianza kufunga lakini Sergio Aguero akasawazishia Argentina.

Wakati huo huo Italia walirekodi mojawapo ya ushindi mkubwa zaidi katika historia ya kufuzu kwa kipute hicho, kwa kuwaadhibu Armenia 9-1.

Shirika la maadili ya wanariadha limefuta marufuku ya mwanariadha wa marathon mkenya Jacob Kendagor. Kendagor alipigwa marufuku kwa kukwepa, kukataa na kukosa kuwasilisha sampuli zake kwa vipimo, ambayo ni kinyume cha kanuni za IAAF za kupambana na dawa za kusisimua misuli. Kendagor hata hivyo alikanusha mashtaka hayo.

Shirikisho la riadha nchini AK limetangaza kuwa majaribio ya Olympiki yatafanyika mjini Eldoret kati ya Juni tarehe 19 na 21 mwakani. Hii itakua mara ya pili majaribio hayo yameandaliwa mjini humo, baada ya kuandaliwa humo mwaka wa 2016. Jana AK ilitangaza kalenda yake ya msimu mpya iliyothibitisha kuwa timu ya Kenya ya Olympiki itaingia kambini ugani Kasarani Juni tarehe 24.