Harambee Stars yakaba Misri koo ugenini, Olunga afunga.

Timu ya Taifa Harambee Stars ililazimisha sare ya bao moja na wenyeji Misri mjini Alexandria katika mechi ya kwanza ya kundi G kufuzu kwa dimba la taifa bingwa barani Afrika mwaka 2021.

Stars walionyesha ujasiri mwingi ugenini. Pharaos ambao walikuwa bila huduma za nyota Mohammed Salah walikuwa wa kwanza kuona lango la Stars dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kupitia mchezaji Mahmoud Kahraba.

Mkufunzi wa Harambee Stars Francis Kimani alilazimika kufanya mabadiliko mawili katika kipindi cha kwanza baada ya mlinda lango Patrick Matasi na winga Ayub Timbe kujeruhiwa na kundolewa wakiwa kwenye machela.

Ian Otieno na Clifton Nyakera waliingizwa kujaza nafasi za Matasi na Timbe mtawalia. Mwanzoni mwa mechi vijana wa taifa walikuwa na wakati mgumu kuhimili miguso ya Pharaos walio onyesha mchezo wa hadhi ya juu wenye pasi kasi.

Mlinda lango wa ziada Ian Otieno alisimama kidete kwenye mikuti huku akipangua mashambulizi ya Pharaos. Ujasiri wake Otieno ulichangia kupanguliwa kwa kombora la Mohamed Abdel Mondem.

Juhudi za nguvu mpya Clifton Nyakera zilizaa matunda baada ya kufuata mpira ulionekana kuelekea nje lakini akaupata ukiwapembeni na kutoa krosi maridadi katika lango la the Pharaos.

Patashika mbele ya lango zilimpa mshambulizi matata Michael Olunga nafasi kupachika wavuni bao la kusawazisha mbele ya maelfu  ya mashabiki wa timu ya nyumbani walioonekana kuvunjika nyoyo.

Stars watarejea nchini siku ya Jumamosi na moja kwa moja kufululiza kambini kujiandaa kwa mchuano wa pili wa kundi G, dhidi ya Togo uwanjani Kasarani.

Togo watakuwa na machungu hasa baada ya kulambishwa sakafu nyumbani na Comoros kwa bao 1-0.