Hasira! Wananchi kuchoma gari la polisi kufuatia ajali ya barabara

Wananchi waliokuwa na gadhabu walilichoma gari la polisi aina ya land cruiser. Hii ni baada ya kuhusika katika ajali na kuwauwa wananchi wanne katika eneo la Kachibora eneo bunge la Cherengany katika kaunti ya Transnzoia.

"Tumehuzunika sana leo kwa sababu barabara hii ya kutoka kachibora kuelekea Kepkeke hakuna matuta (bumps),

"Ajali zimekuwa zikitendeka hapa kila siku, juzi mtoto aliweza kugongwa katika barabara hii, tumeweza kuzika watu wengi kwa ajili ya barabara hii,

"Ata mimi nilikuwa karibu kugongwa katika barabara hii, kwa hivyo tunawauliza polisi wa eneo hili waache kukimbilia hongo na kuenda kwa chang'aa na pia kwa watu wa pikipiki jameni! mnataka tuishi aje? Alizungumza Mkazi wa Kachibora.

Kizaazaa hicho kilizuka baada ya gari hilo kuhusika katika ajali na pikipiki iliyokuwa imewabeba mama na watoto wawili huku watoto wakiaga dunia baada ya kufikishwa katika hospitali ya Cherengany, kaunti hiyo ya Transnzoia.

Hatua ambayo ilichangia wananchi kuchukua hatua ya kulitekeleza gari hilo la polisi huku wakiwalaumu maafisa hao wa polisi kwa ajali hiyo.

"Tumepoteza jamii kutoka eneo hili, tuna upetepetu katika sehemu zetu za kaunti kwa maana gari la kuzima moto limekuja likuwa limechelewa,

"Limewasili wakati ambao kitendo hicho kimetendeka na pia moto ulikuwa ushaazimika, polisi pia waliweza kuchukua muda mrefu kufika mahali hapa," Alisema Gerald Babu.

Hata hivyo naibu kamishna wa kaunti ya Transnzoia katika kata ndogo ya Cherengany Calistus Kendi, aliweza kuwaomba wananchi kuacha kujichukulia hatua mikononi wakati hali kama hiyo inatokea.

"Ajali hiyo imeweza kusababisha vifo vya watu wanne watoto wawili, mama yao na mwendeshaji pikipiki, ni kama mwendeshaji pikipiki aliweza kupoteza mwelekeo kisha ajali hiyo ikatokea,

"Ninajua wananchi wana uchungu mwingi sana kwa maana gari moja ya polisi imeweza kuchomwa, waathiriwa hao walikimbizwa katika hospitali ya Cherengany lakini kwa bahati mbaya wameweza kufariki," Alieleza Calistus.

Huku akisema maafisa wa polisi wanaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.