Hatma ya kocha wa Gor Mahia haijulikani baada yake kuondoka nchini

Hatma ya kocha wa Gor Mahia Hassan Oktay bado haijulikani baada yake kuondoka nchini jana kushughulikia suala la kibinafsi kwao Uturuki.

Ingawaje klabu hiyo ilitangaza kwamba kocha huyo ataregea, kuna ripoti kua huenda Oktay hatarudi baada ya kukosana na usimamizi wa klabu hiyo baada ya kusajili wachezaji kadha bila ya kumhusisha.

Klabu hiyo pia ilipoteza wachezaji kadhaa nyota wa hivi majuzi akiwa Haron Shakava kabla ya msimu mpya kuanza.

Kwingineko, kundi la kwanza la timu ya kinadada ya Voliboli liliondoka nchini jana kuelekea Italia ambapo watashiriki michuano ya kufuzu kwa olimpiki ya mabara.

Kundi hilo lilijumuisha wachezaji 7 na kocha Japheth Munala. Haijabainika ni kwa nini timu hiyo ilibidi kusafiri kwa makundi mawili huku kundi la pili likitarajiwa kuondoka leo ikizingatiwa kwamba michezo hiyo inaanza hapo kesho.

Ifuatayo ni msururu wa ripoti za soka duniani.

Harry Kane alifunga bao la pekee, Tottenham walipowanyuka Real Madrid 1-0 katika nusu fainali ya kombe la Audi. Mshambulizi huyo wa Uingereza alichukua fursa ya mkanganyiko katika safu ya ulinzi ya Real na kufungua bao baada ya dakika 22.

Licha ya kuwepo kwa nafasi zingine za kufunga Spurs walistahimili shinikizo kutoka kwa Madrid na kufuzu kwa fainali kabla ya kuialika Inter Milan kwa kombe la kimataifa la mabingwa jumapili mchana. Klabu hiyo kisha itaanza msimu wa ligi ya Premier kwa kuchuana na Aston Villa.

Agenti wa Paulo Dybala yuko jijini London kwa mazungumzo na Manchester United kuhusu mkataba wa kubadilishana na Juventus na Romelu Lukaku.

Hatma ya Dybala imekua ikijadiliwa hivi majuzi huku United wakiwa tayari kumsajili kiungo huyo raia wa Argentina kama makubaliano ya Lukaku kuondoka Old Trafford yakionekana kuwa karibu kuafikiwa. Inaaminika kwamba majadiliano hayo yako katika kiwango cha awali na hakuna hakikisho kua United itatoa ofa kumsajili kiungo huyo ws Argentina, au hata iwapo anataka kuhamia Old Trafford.

Lukaku pia anamezewa mate na Inter Milan, ingawaje hawajafikia thamani ya United ya mshambulizi huyo wa Ubelgiji.

Mashabiki wa Korea Kusini waliojawa na ghadhabu wanataka warudishiwe hela zao baada ya Cristiano Ronaldo kushindwa kuingia uwanjani wakati wa mechi ya kirafiki ya kabla ya msimu dhidi ya Juventus.

Nyota huyo wa Ureno alikuwa ametia saini mkataba wa kucheza dakika 45 wakati mechi dhidi ya timu hiyo ya Ligi, ya nyota wote ilipotangazwa kulingana na waandalizi, lakini alikaa kwenye benchi nje ya uwanja.

Mashabiki hao walianza kutaja jina hasimu wake Lionel Messi, ilipodhihirika kua hataingia uwanjani.