Hekaya za Natembeya! Kijana aliyejibizana na Natembeya arejesha silaha

Mvulana wa miaka 13 aliyemshangaza mratibu wa Bonde la Ufa George Natembeya kwa kumuuliza maswali mazito amesalimisha silaha zake.

Kijana huyo aliyerejesha silaha hizo Jumatano, Juni 3 alitii amri ya Natembeya iliyowataka watu wa jamii ya Kipsigis na Maasai kusalimisha bunduki na silaha zingine walizomiliki kinyume na sheria.

Kwenye ripoti ya Citizen TV, mvulana huyo pia alihubiri ujumbe wa amani huku akiwashauri vijana wenzake katika maeneo hayo kuzika uhasamana na kurejea shuleni.

"Ninawasihi vijana wasijiingize katika vurugu, hayo tumesuluhishia hapa leo na bado tunaendelea na harakati za kuzisalimisha silaha. Tunapaswa pia kurudi shuleni," alishauri kijana huyo.

Awali, kijana huyo aliyekuwa na ghadhabu alidai alikuwa akiipigania familia yake baada ya nyumba yao kuteketezwa katika mzozo wa kikabila huko Ololompanki na Oloruashi Narok.

Mamake kijana huyo alisema hakujua alikokuwa mwanawe baada ya vita kuzuka na alipigwa na butwaa kumuona kwenye Runinga.

Video ya tukio hilo iliibuka mtandaoni Jumatano, Mei 27 na kuonesha Natembeya akimuita kijana huyo kutoka kwenye umati kabla ya kuanza kumuhoji katika baraza la usalama lililokuwa limeandaliwa.

"Huyu kijana nilimuona kwa runinga akiwa na mishale. Kijana kama huyu akilelewa kwa mazingira kama haya atakuwaje?"  Alisema Natembeya,