Hii Itaweza? Ruto aunda mkakati wa 2022 ili kuzichukua ngome za Uhuru, Raila

Naibu wa rais William Ruto  anaunda mkakati  kabambe wa kuweza kuzichukua  ngome za rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi mkuu ujao. Sehemu ya mpango huo imeanza kutekelezwa  kwa kutoa taswira kwamba  kipute cha kuwania urais ni kati ya maskini na walioavyo  kwa ufupi kwamba mahustler watakuwa upande mmoja ilhali watoto wa familia za ‘kifalme’ watakuwa upande wa pili.

Naibu wa rais amekuwa akijitangaza kama sauti na mtetezi wa watu maskini  na ameamua kuzungumza moja kwa moja na wananchi huku akimuacha Uhuru kusalia kama kiongozi  mwenye mamlaka yanayoonekana ya kurithi kutoka kwa familia. Wanaomshauri Ruto wanaamini kwamba anaweza kupata kura za kutosha katika maeneo ya kati, Lower Eastern, Magharibi, Pwani  na Kaskazini  mashariki ili kuchukua hatamu za uongozi mwaka wa 2022.

DP ambaye ametimuliwa kutoka ngome za mamlaka  amekuwa akitoa misaada kwa biashara ndogo ndogo ili kujitangaza kwamba anayajali maslahi yao  na kupandisha hadhi yake machoni pa watu wengi wa kawaida. Wanaojua undani wa mango huo wanasema  washirika wa Ruto wamechakura utafiti wa shirika la takwimu nchini kuhusu mambo ya uchumi na wanatumia takwimu hizo ili kujua kero za wananchi na kuahidi kuzishughulikia kupitia njia mbalimbali ikiwemo kuwapa misaada inayotolewa na kambi ya Ruto.

Kwa mfano ripoti hiyo iligundua kwamba maeneo ya Mlima Kenya,Nairobi, Nyanza  na Rift Valley yana idadi ya juu ya wafanyibiashara wadogo wadogo.  Walifaulu katika shughuli zao bila kutegemea  utajiri wowote wa kifamilia  na wanakumbana na changamoto nyingi sana  ikiwemo kunaswa kwa  mali za wafanyibiashara wengi wanaoagiza bidhaa kutoka nje katika msako dhidi ya bidhaa za ubora wa chini ama ghushi, kundi la Ruto linategemea  kutumia malalamishi kama hayo ili kujenga uungwaji mkono miongoni mwa watu. Washirika wa Ruto wanasema baadhi ya biashara zinatoa upinzani kwa zile zinazomilikiwa na  watu kutoka familia  zenye ushawishi mkubwa kisiasa  na ndio kwa sababu zililengwa na mashirika ya serikali. Mbunge wa Belgut Nelson Koech  ambaye ni miongoni mwa wanaofanya kazi kwa karibu sana na DP ameliambia gazeti la The Star kwamba  vuguvugu la ‘hustler Nation’  litakuwa kubwa kuliko  migawanyiko ya kikabila  bali litategemea  dhana na fikra za kibiashara  miongoni mwa wakenya .

Washirika wa Raila hata hivyo wamepuuza mbinu hiyo ya Ruto  wakisema haitamsaidia Ruto kupata kura katika uchaguzi mkuu ujao. Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi  ameutaja mkakati huo kama wa ‘kushangaza kwa sababu hauna nafasi katika  siasa za Kenya’.