Huenda utalipa zaidi kwa safari yako ya bodaboda

Huenda ukalazimika kulipa zaidi kwa safari yako ya boda-boda iwapo wabunge watayakubali mapendekezo ya waziri wa fedha Henry Rotich kwamba ni lazima wawe na bima ya wateja wao.

Anasema hii ni muhimu katika kuthibiti ajali zinazosababishwa na vyombo vya usafiri. Mbunge wa Alego Usonga Sam Atandi hata hivyo ameapa kulipinga pendekezo hilo.

Kwingineko, maafisa wa serikali sasa hawatapokea marupurupu wakiwa katika shughuli za kikazi humu nchini na nje ya nchi. Waziri wa fedha Henry Rotich jana alisema kua kama mojawapo ya mikakati ya serikali ya kupunguza matumizi ya serikali, kutakua na mfumo wa kadi ya kielektroniki ili kupunguza ubadhurufi wa fedha za umma.

Bado katika maswala ya bajeti, serikali inapanga kutumia shilingi bilioni 326 kwa usalama wa taifa katika bajeti ya mwaka 2019/2020. Rotich anasema usalama wa taifa ni nguzo muhimu ya uthabiti wa kiuchumi na huchangia pakubwa kuvutia wawekezaji.