Ilikuaje: Maisha ya umaskini ndio yalinipa motisha - Millicent Ntinyari

Mwanadada kwa jina Millicent Ntinyari, amekuwa nguzo kuu kwa vijana wengi nchini hii ni baada ya mwanharakati Boniface Mwangi kueneza habari kumhusu.

Boniface Mwangi alishangazwa na jitihada za mwanadada huyo kwani anafanya kazi kadhaa kama dereva wa texi, kuuza nguo za kina dada na pia kazi ya Cabin Crew.

Isitoshe, Ntinyari ni mama wa mtoto mmoja wa miaka miwili na pia mwanafunzi.

Mwangi aliandika katika mtandao wake Instagram,

My taxify driver was Ntinyari Rutere, works as cabin crew at Wilson Airport, goes for evening classes, she is doing her undergrad in corporate communications and sells clothes.

Ntinyari ndiye alikuwa mgeni wetu katika kitengo cha Ilikuaje kinacholetwa na Massawe Japanni na alisimulia kuwa walilelewa katika maisha magumu, na hilo ndilo lilimpa motisha kufanya kazi kwa bidii.

Lakini je yeye huwezaje kufanya hayo yote?

Kazi yangu inaniruhusu kufanya biashara, kuwa dereva, kufanya deliveries, jioni naenda darasani na somo likiisha mapema nafanya kazi ya udereva lakini wikendi nampea mtoto wangu mda.

Watu shida hawakuwa wanaelewa kuwa sifanyi na huduma za ndege za kimataifa bali ni hapa nchini, kwa hivyo nina wakati wa kulea mtoto na kufanya biashara.

Wazazi wake walitengana akiwa mdogo na walilelewa na mama wa kambo ambaye aliwatesa jambo ambalo liliwacha hasira na uchungu mwingi moyoni.

Nimetoka kwenye familia ambayo hatukuwa na uwezo kwani shida kuu wazazi wangu walitengana nikiwa darasa la tano. Hapo tukapata step mother ambaye alikuwa anatutesa na nilikuwa kama mama mzazi kwa dadangu.

Sasa hilo ndilo lilinipa motisha ya maisha kwani nilisema nikisoma hapo ndio nitabadilisha maisha yetu.

Nilipata mtoto na hapo ikawa nikama nina watoto wawili, mimi na dadangu.

Hata hivyo, Ntinyari bado ana uchungu mwingi kila anapomkumbuka marehemu babu yake ambaye aliwalea yeye na ndugu zake pindi wazazi wake walipotengana.

Anasema kuwa babu yake alikuwa amemuahidi kuwa atamlipia karo ya shule ya upili lakini kwa bahati mbaya akaaga dunia.

Nilibaki na uchungu mkuu kwani nilijiuliza kama singekuwa na babu yangu tungekuwa wapi halafu unajua yule mama wa kambo aliniwacha na alama kichwani.

Halafu babu yangu alifariki pindi tu nilipomaliza darasa la nane na niliumia sana kwani alikuwa ameniahidi kuwa atanipeleka shule.