Ilikuaje: Ndoa ni jinsi wewe unavyotaka iwe - Janet Otieno

Msanii Janet Otieno ni mmoja wa wasanii wa injili wanaosifika sana humu nchini na ambaye anaheshimika zaidi, hii ni kwa jinsi anavyo jibeba na pia ujumbe anaoeneza kupitia talanta yake.

Leo katika kitengo cha Ilikuaje, naye Massawe Japanni, Janet, alizungumzia maswala mengi yakiwemo ya ndoa yake na jinsi ya kuifanya ndoa yako iwe ya kutamanika.

Janet ambaye ameolewa kwa miaka ishirini na mitatu, anasema kuwa ndoa ni vile wewe utakavyotaka iwe kwani watu au pia ndoa hazifanani.

Ndoa yako ni wewe na jinsi unavyotaka iwe kwani watu tofauti ndio hupatana na kwanza maisha. Watu wanapaswa kuzungumza na wajaribu kuvumilia sio kuruka kutoka ndoa hii hadi nyingine.

Anasema kuwa yeye hapendelei kuona ndoa zikivunjika kwani wanandoa wanapaswa kuvumiliana na kuhakikisha kuwa mazungumzo yao ni ya hali ya juu.

Hata hivyo, aliongeza kuwa kama ndoa ina vita na mateso hapo hawezi shauri yeyote kubakia pale.

Mie sipendelei watu watengane ila ikafikia mahali unapigwa na kuteswa hayo ni mambo mengine lakini watu wajifunze kuvumiliana na kuwasiliana.

Janet anatambulika sana kwa ngoma kama Napokea kwako, uniongeze na tulia sasa ana wimbo mpya uitwao pokea.

Akisimulia kilichompa hamasisho ya kuutunga, alisema alipata wito akiwa nchi ya uholanzi ambapo sauti ya mungu ilimpa ujumbe.

Nakumbuka nilikuwa nangoja mungu anionekania katika jambo fulani na ni kama alikuwa anachukua mda sana. Sauti ilinijia na kunikumbusha kuwa nafaa kumshukuru mola kwa kila kitu kwani shukran hufungua milango mingi.