Ilikuwaje: Mamangu mzazi alinitekeleza na kumpendelea dadangu

Mama mmoja ameelezea jinsi mamaye mzazi alivyomtekeleza maishani mwake akiwa katika shule ya msingi huku kisa na maana ikiwa ni kushindwa kufanya vyema shuleni. Doreen kwa sasa ni mama wa mtoto mmoja na anaishi mjini Nairobi kwenye harakati za kumtaftia mwanawe riziki.

"Tulizaliwa tukiwa wasichana wawili. Mamangu alikuwa anapenda dadangu mdogo kuniliko kwa sababu alikuwa mwerevu darasani. Mama aliakuwa ananidharau sana hadi kiasi kwamba aliacha kunilipia karo shuleni."

Doreen amelezea Masawe Japani kuwa mamaye alikataa kumlipia karo ya shule jambo lilompea mawazo mengi maishani. Baba yake doreen na mama yake walitalikiana akiwa mdogo hivyo mamake ndio alikuwa mlezi wa kipekee.

"Niliamua kumwitisha baba karo baada ya mama kukataa kunilipia ila baba alinituma kwa mama nimuulize kama anakubali baba anilipie karo. Nilimbebeleza mama akubali nilipiwe karo ila alikataa na kusema kuwa haina haja kuharibu pesa kwa watoto wajinga shuleni."

Ukali wake mamaye ulimpelekea Doreen kumuuliza mamaye mzazi iwapo yeye alikuwa mmoja wa watoto wake." Baba na mama walirudiana na nilipowauliza kuhusu hatma yangu shuleni walikata hadi mama akaniambia mimi ni wale watoto hufanya mapenzi na baba zao jambo lililoniudhi sana moyoni mwangu."

Kutokana na matatizo haya, Doreen alianza kufanya kazi ya vibarua ili aweze kupata pesa za karo yake huku dadake mdogo alikuwa analipiwa karo na wazazi wao. Doreen alimaliza darasa la nane akiwa na umri wa miaka kumi na minane huku dadaye alikuwa tayari amekamilisha masomo ya shule ya msingi na alikuwa katika shule ya upili.

" Baada ya miaka kadha ilinibidi niolewe ili niweze kukidhi mahitaji yangu. Niliachia masomo baada ya kumaliza shule ya msingi ila dadangu alilipiwa karo hadi akamiliza kidato cha nne. Hata hivyo,ndoa yangu haikukawia sana kwani ilivunjika na nilipozungumza na mama aliniambia nisimpelekee mtoto kwake."

Kwa sasa Doreen ni anaishi hapa mjini Nairobi na jambo kubwa yeye hushirikiana na mamaye mzazi ni salamu pekee kwani hadi leo hii mamaye hampendi kamwe.