IPOA yachunguza ukatili wa pilisi katika City Hall

Mamlaka huru ya shughuli za polisi (IPOA) imeanzisha uchunguzi kuhusiana na madai ya dhulma za polisi katika City Hall mjini Nairobi siku ya Jumanne.

Mwenyekiti Anne Makori siku ya Jumanne alisema kwamba mamlaka hiyo tayari imewasiliana na watu waliokuwepo wakati wa ghasia zilizoshuhudiwa katika bunge la kaunti ya Nairobi mapema siku ya Jumanne.

Soma habari zaidi;

"Uchunguzi huu wa awali unalenga kubainisha hatua ya polisi waliotumwa kushika doria ghasia zilipozuka na ambapo kesi moja ya kujeruhiwa kwa mwakilishi mmoja wa wadi iliripotiwa," Makori alisema.

Makori aliongeza kuwa watahakikisha kwamba polisi hawatumii nguvu kupita kiasi kila wanapotuliza ghasia na kwamba tukio lolote ambapo polisi wanatumia nguvu kupita kiasi na kinyume na sheria hatua kali zitachukuliwa dhidi ya maafisa husika.

"Mamlaka hiyo ni huru na haiegemei upande wowote katika kutekeleza uchunguzi dhidi ya malalamishi yaliowasilishwa kwake," alisema.

Soma habari zaidi;

Mwakilishi wadi wa Mlango Kubwa Patricia Mutheu anadaiwa kucharazwa marungu na kudhulumiwa na polisi baada ya ghasia kuzuka katika City Hall.

Hii ni baada ya kundi moja la wakilishi wadi kujaribu kumpokeza Spika Beatrice Elachi notisi ya hoja ya kutaka kumfurusha iliokuwa imetiwa saini na wakilishi wadi 59.

Kulikuwepo idadi kubwa ya polisi waliozuia wakilishi wadi hao ambao pia walitaka kumkabidhi Elachi agizo la mahakama kuzuia uteuzi wa Edward Gichana kama karani wa bunge la kaunti ya Nairobi.

Soma habari zaidi;

Hata hivyo Elachi alijiufungia afisini mwake huku polisi wakizuia wakilishi wadi hao dhidi ya kufikia afisini mwake.

Mutheu alisema kwamba alitandikwa na polisi alipokaidi amri ya kuondoka baada ya ghasia kuzuka bungeni.