Je shule na makanisa nchini zitafunguliwa? Rais Kenyatta ataka wizara ya Elimu na Usalama kushirikiana

Akitoa hotuba yake kwa taifa wakati wa maadhimisho ya siku ya Madaraka kwenye ikulu ya Nairibi, kiongozi wa Kenya Uhuru Kenyatta amezitaka wizara mbili za Usalama na Elimu kumalizia mashauriano baina ya washikadau husika katika sekta hizo mbili.

Katika hotuba yake hiyo, kiongozi wa taifa amesema anawasikitikia wanafunzi ambao wanapaswa kufanya mitihani yao ya kitaifa mwaka huu baada ya shule kufungwa kighafla kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona.

Wizara ya usalama wa ndani inatarajiwa kuandaa kikao na washikadau nchini wa makanisa na madhehebu mengine ili kutoa vigezo vitakavyofuatwa na wahumini wa makanisa tofauti nchini.

Wakati uo huo kiongozi wa taifa vile vile ameitaka hazina ya kitaifa kutoa shilingi bilioni 2 ili ziende katika sekta ya hoteli nchini [Hospitality] baada ya sekta hiyo kuendelea kuumia kutokana na hasara iliyosababishwa na virusi hivyo.

Wito huo wa rais Kenyatta unajiri siku chache tu baada ya hoteli za Serena na Fairmont kutangaza kuwafuta wafanyakazi wake wote.