Je, Mudavadi anajua anataka nini? Hofu ya kujipata katika njia panda yazuka kabla ya uchaguzi wa 2022

Hofu ya uwezekano wa kujipata katika njia panda  kabla ya uchaguzi  mkuu wa 2022 imeibuka katika kambi ya Musalia Mudavdi  huku washirika wake wakuu wakitoa jumbe zinazokinzana kuhusu mipango yake ya 2022 .

Hali hiyo imeleta hali ya  mkanganyiko katika mrengo wake  na kwenye uongozi wa ANC  huku Mudavadi akisema yuko tayari kumrithi rais Uhuru Kenyatta.

Kiongozi huyo wa ANC  amezidisha shughuli zake za kisiasa  lakini wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kambi yake bado ina mgawanyiko na haijafanya uamuzi thabiti kuhusu  uchaguzi huo.

Kwa upande mmoja kuna washauri wake wanaomataka ajiunge na  kambi ya naibu wa Rais Willian Ruto, kwa upande mwingine  baadhi ya washirika wake wanamtaka amkaribie rais Uhuru Kenyatta ili aweze kumtaja kama mrithi wake na pia kupiga jeki juhudi zake za kutaka kuwa rais.

Mwaka wa 2002,  Mudavadi alikaidi  wimbi la upinzani Narc na kumuunga mkono  Uhuru Kenyatta  na chama cha Kanu  walioshindwa katika uchaguzi huo licha ya kuungwa mkono na rais Daniel Moi.

Aliyekuwa waziri Franklin  Bett  ameliambia gazeti la The Star kwamba ingawaje Mudavadi ni mwanasiasa  stadi, hajaweza kujitokeza kwa ukakamavu kupigania nafasi yake kuchukua usukani katika siasa.

" Wimbi la 2022 linaonekana kuwaegemea wale wanaounga mkono mwafaka wa BBI’ amesema Bett .

Hata hivyo  naibu kiongozi wa chama cha ANC  Ayub Savula  amesema Mudavdi anasalia mgombeaji thabiti wa kuchukua nafasi ya urais katika uchaguzi  mkuu wa 2022.