Jua jamaa zako! Mtu amuuoa dadake na hata kupata mtoto naye

Family Reunion
Family Reunion
Mambo ya kuishi mjini kwa muda mrefu bila kuweka mikakati ya kuwatembelea jamaa zako mashambani yana matokeo  ambayo si mazuri.

Najua ni vigumu kwenda mashambani kila wakati  iwapo safari hiyo inachukua siku nzima kwenda na nyingine kurejea  na ndio maana kuna  mwezi wa Disemba - likizo ndefu  ambayo watu wanafaa kutangamana na familia zao katika sehemu mbali mbali za nchi na dunia nzima.

Ni bora kuandaa angalau hafla ya kutangamana kama familia ‘family Reunion’ kila mwaka ili watu wajuane na kuepuka masaibu yaliowakumba watoto wawili wa baba mmoja na mama tofauti ambao waliooana huko Mombasa bila kujua kwamba baba yao ni mmoja! mwaka wa 1996  Jerry  Kinuthia na Jane Mwangi walikutana Vipingo.

Kimoja baada ya kingine basi wakawa  washaamua kuwa wapenzi na kupiga kila hatua ya kuishi kama mke na mume. Jane  alijua babake alitengana na mamake miaka mingi  wakati alipokuwa mdogo na  hakuwahi kumuona tangia hapo. Jerry  naye alimjua babake kwa sababu mamake alikuwa mke wa pili baada ya kuambiwa mke wa babake wa kwanza alitoroka zamani baada ya mamake na babake kukutana. Mzee wa watu alikuwa akifanya kazi na shirika la reli na  baada ya kustaafu akarudi zake Thik  ,kumbe kaacha mbegu huko Mombasa.

Watoto walikutana wakiwa watu wazima na kama  ilivyo ada ya vijana wa karne hii wanajifanyia mambo bila hata kuwashauri wazee kisha baadaye yanapozidi  maji ndio sasa wanawaambia wazee.

Miaka miwili wakiishi kama mume na  mke,Jerry na Jane hawakuwa na mbio za kutambulishana kwa familia zote na wakati wanapokutana na familia ya mwingine ilikuwa tu kwa mapito tena mbio mbio lakini siku yao ilifika  mwaka wa 1998 .

Kutokana na shambulizi la kigaidi mjini Nairobi mwaka huo, Hoteli nyingi huko pwani zilijipata bila wateja na kulikuwa na hofu ya wageni kuja nchini. Hoteli nyingi ziliamua kuwafuta kazi wafanyikazi wake lakini Jerry na Jane walipewa muda wa kupumzika hadi hali iboreke kisha wangerejea kazini baada ya miezi miwili hivi. Kwa sababu likizo hiyo haikuwa katika mpango wao waliamua basi wataitumia kuja Thika kwa babake Jerry ili aweze kumtambulisha mkewe na mtoto wao ambaye wakati huo alikuwa na umri wa mwaka mmoja.

Safari ya kuja Thika ilifanikishwa na  familia ya Jerry ilikuwa sana na furaha ya kumkaribisha mkaza mwana wao kutoka Mombasa, ingawaje alikuwa anafahamu lugha ya kikuyu lakini baada ya kuzaliwa na kukulia pwani, ilikuwa vigumu sana kujua kwamba chimbuko lake ni Kati mwaka Kenya.

  

Kishindo kilianzia tu siku waliofika mtaa wa Makongeni Thika wakati Mzee  alipomwona   Jane, ingawaje macho yalikuwa yameanza kumfelisha kwa sababu ya umri, Mzee alishangaa kumuona Yule binti ambaye alikuwa akifanana sana na mkewe wa kwanza waliyekutana naye Mombasa miaka ya nyuma! Mzee baada ya salamu  hakutulia.

Alitaka kwanza kumjua Jane na akaanza kumuuliza swali baada ya jingine. Mama mkwe alihamakishwa na msururu wa maswali hayo na akamkatiza Mzee akimuambia awape watoto muda wa kutulia kwanza nyumbani kisha angeendelea na maswali yake baadaye. Wakati  familia nzima ilipokuwa mezani kwa chakula,mzee alikuwa katika lindi  la mawazo na wote walishuhudia jinsi akili zake zilikuwa mbali.

Walishangaa kimemfanyikia nini Mzee hasemi lolote ? Baadaye Mzee alimuita mwanawe na mke wake kisha akawaambia kuna jambo ambalo limefanyika visivyo. Alisema Jane ni dadake Jerry kwa sababu  maelezo yake yote yamethibitisha kwamba mamake Jane ni mke wake wa kwanza waliyetangana naye huko Mombasa. Mzee alijutia kilichofanyika na kuwaambia kwamba makosa hayakuwa yao na kwamba ndiye anayefaa kulaumiwa  kwa sababu angechukua  juhudi za kuzileta pamoja familia zao. Mtu na mke wake walipatwa na butwaa na hawakuamini kwamba walikosa kugundua mapema kwamba walikuwa mtu na dadake .

Kizungumkuti kilizuka wakati Jane na Jerry waliposema kwamba kamwe  hawatatotengana. Familia nzima ilishangaa na ilishindwa itashughulikia vipi  suala hilo. Waliogopa sana watu wa nje wafahamu kwamba watoto wao wawili waliooana bila kujua na hata wakampata mtoto.  Familia na wazee walisema kwamba lazima Jerry na Jane watengane lakini nao walipinga hilo. Keshoye waliondoka kurejea Mombasa na haikufahamika iwapo baadaye walifuata ushauri wa kuivunja ndoa yao hiyo .