Jurgen Klopp adokeza huenda akaondoka Liverpool mkataba wake ukikamilika

jurgen.klopp
jurgen.klopp
Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp amedokeza kwamba huenda akaondoka klabu hio atakapomaliza mkataba wake wa sasa.

Meneja huyo wa zamani wa Borussia Dortmund alijunga na Liverpool mwaka wa 2015 na kwa sasa ana mkataba hadi mwaka wa 2022. Wamilikiwa Liverpool Fenway sports Group wanamtaka Klopp kusalia humo lakini mjerumani huyo anataka kuondoka, mkataba wake utakapokamilika katika muda wa miaka mitatu ijayo.

Aliyekuwa nahodha Steven Gerrard ametajwa kuwa huenda akachukua mahala pa Klopp.

Vilabu vya ligi ya Premier vitajadili iwapo vitabadilisha makataa ya dirisha la uhamisho la msimu wa joto mwezi ujao. Dirisha la uhamisho la msimu huu wa joto lilifungwa masaa machache kabla ya mechi ya ufunguzi kati ya Liverpool na Norwich ugani Anfield. Vilabu hivyo vitakutana Septemba tarehe 12 kwa majadiliano hayo, ingawaje hakuna uhakika wa iwapo kutapigwa kura.

Huenda Manchester United ikasubiri ukaguzi wa mchezaji wa kiungo wa mbele raia wa Ufaransa Anthony Martial, mwenye umri wa miaka 23, kabla ya kuruhusu uhamisho wa mkopo wa mchezaji wa kimataifa wa Chile Alexis Sanchez, mwenye umri wa miaka 30, kwenda Inter Milan.

Wakati huo huo Mchezaji wa kimataifa wa Serbia Nemanja Matic, mwenye umri wa miaka 31, ameitisha mazungumzo na Ole Gunnar Solskjaer baada ya kuipoteza nafasi yake ya kwanza huko Old Trafford.

Romelu Lukaku alifungia Inter Milan katika mechi yake ya kwanza ya Serie A walipowanyuka Lecce (LECHE) mabao 4-0. Mshambulizi huyo raia wa Ubelgiji aliyesajiliwa na Inter kwa kitita cha Uro milioni 80 kutoka Manchester United mwezi uliopita alifunga bao la tatu kunako dakika ya 60.

Marcelo Brozovic alifungia Inter bao la ufunguzi huku Stefano Sensi akifanya mambo kuwa 2-0. Bao la Antonio Candreva lilikamilisha ushindi wao.