Kafyu ya mauti! Mhudumu wa boda boda apoteza maisha yake akihepa maafisa wa polisi

Familia moja Kaunti ya Kilifi inaomboleza kifo cha mpendwa wao ambaye alipoteza maisha yake akiwatoroka maafisa wa polisi.

Inadaiwa kwamba polisi walikuwa wakimkimbiza Karissa Nguwa ambaye ni mhudumu wa boda boda, mnamo Jumamosi, Juni 6, mwendo wa saa moja unusu usiku na kuamua kujirusha ndani ya mto.

Kulingana na rafiki yake wa karibu aliyeshuhudia kisa hicho, kabla ya mwendazake kujirusha ndani ya mto, alikuwa amepigwa na maafisa hao kwa kukiuka sheria za kafyu.

Rafiki yake alikuwa na wasiwasi wakati Karissa alichukuwa muda mwingi kujitokeza baada ya polisi hao kuondoka na piki piki yake kama ilivyoripoti CitizenTV.

"Wakati walifika mtoni, walikutana na maafisa wa polisi ambao walikuwa wameshika doria. Polisi waliwasimamisha lakini waliogopa."

"Walianza kuenda katika upande tofauti. Polisi walianza kuwakimbiza na mmoja alikamatwa. Wakati alishuka kutoka kwa pikipiki, walimchapa.Wakati aliruka ndani ya mto, polisi waliondoka na pikipiki yake. Mwenzake alianza kumuomba aondoke mtoni lakini hakutoka." alisimulia shahidi huyo.

Mjane wake Karisaa aliomba serikali kumsaidia kwani mume wake ndiye alikuwa tegemeo kwa familia hiyo ya watoto wanne.

"Ninaomba msaada. Nina watoto wanne na mjukuu mmoja na ninataka mume wangu afanyiwe haki," alisema mjane huyo.

Haya yanakujia siku chache baada ya Halmashauri Utathmini wa Utendakazi wa maafisa wa Polisi (IPOA) kutangaza majina ya maafisa sita wa polisi ambao wamepatikana na hatia ya kutenda dhuluma dhidi ya raia.

Katika taarifa siku ya Alhamisi, June 4, kupitia Twitter, halmashauri hiyo ilimpa idhini Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ya kufungua kesi dhidi yao kwa madai yanayowakabili.

Miongoni mwa maafisa hao ni wanaotarajiwa kukamatwa ni pamoja na aliyempiga risasi na kumuua kijana Yassin Hussein Moyo, aliyekuwa amekaa roshani ya nyumbani kwao katika mtaa wa Kariobangi, usiku.