Kamanda wa Alshabab katika shambulizi la basi Wajir alikuwa mwalimu mkuu

Medina Bus
Medina Bus
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi anadaiwa kuongoza kikosi cha wanamgambo wa Ashabab walioshambulia basi la Medina na kuwauwa abiria 11 Wajir.

Kulingana na idara ya polisi, Mohammed Hussein Hassan anasemekana kutorokea Somalia baada ya serikali kuwatuma vikosi vya walinda usalama kuwasaka  wanamgambo hao.

Maafisa wanane wa kikosi cha kupambana na wizi wa mifugo na raia watatu ni miongoni mwa abiria 56 waliokuwa katika basi la Medina walipotengwa na kuawa na majangili hao.

"Walikuwa wamearifiwa kuwa basi lilikuwa linawasafirisha  maafisa wa polisi kuelekea vituo vyao vya kazi," afisa mmoja alisema.

Aidha, taarifa za upelelezi zinasema kuwa huenda kuna baadhi ya abiria walioshirikiana na wanamgambo  kutekeleza shambulizi hilo.

Taarifa za kijasusi zinasema kuwa baadhi ya wapiganaji hao wa Alshabab waliingia nchini Novemba na wamekuwa chini ya mwalimu huyo mkuu.

Mnamo Jumapili, kamishina wa kanda ya Kaskazini Mashariki, Mohamed Birik alisema kuwa washukiwa 11 wametiwa mbaroni.

"Tutawachukulia hatua kali familia na watu waliwapa makazi wapiganaji hao," Birik alisema.

Hata hivyo maisha ya maafisa hao yangeokolewa iwapo wangesafiria Land Cruiser ya polisi kwa kuwa kulikuwa na mafuta ya gari ya  kutosha kuwasafirisha kutoka Elaraham.

Inasemekana kuwa maafisa hao walikuwa wameshauriwa kuchangisha pesa za kununua mafuta ya gari lakini  wakakataa na wakaamua kusafiria basi hilo.

Katika taarifa za rais kutoka msemaji wa serikali Kanze Dena Jumamosi, rais Uhuru Kenyatta alionya kuwa kundi la Alshabab halitasaswa.