KCSE: Magoha awaonya wazazi wanaopanga kununua mitihani

Watahiniwa wa KCSE watakao shiriki katika wizi wa mitihani hawatapata matokeo yao, waziri wa elimu, George Magoha amesema.

Hii inafuatia ripoti kuwa wazazi kadhaa kutoka Migori, Kisii na Homa Bay wamechangisha fedha nyingi kulipa maafisa wa mitihani ili kuwezesha wizi wa mitihani.

Magoha anasema kuwa waliopanga njama hiyo wamemtambua msimamizi ambaye alikuwa alipwe, Sh120,000, msimamizi mwingine Sh60,000 na afisa wa polisi Sh40,000.

Hata hivyo ameonya kuwa hatua imechukuliwa na waliohusika watambana na nguvu kamili ya sheria. Magoha aliwaomba watahiniwa kutokubali kujihusisha na makosa hayo.

"Usidanganywe na watu wazima ambao hawana hekima, usiseme kuwa hukuonywa." Waziri huyo alisema.

Aliwaambia wanafunzi kutokubali "Usaidizi kutoka jehanamu" bali wakubali usaidizi kutoka binguni.

Magoha alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa wazazi kadhaa wanaokota fedha nyingi ili tu walipie mitihani.

"Nilidhani tulitoka kwa mambo kama haya. Hatua kali zitachukuliwa," aliongeza.

Alikuwa anazungumza akiwa Kisumu Jumapili alikokuwa akisimamia ufunguzi wa konteina ya mitihani kabla ya kusambazwa.

-The Star