Ken Okoth, mahakama yaruhusu kufanyika kwa mazishi yake

ken.son.1
ken.son.1
Mahakama ya Kilimani imeruhusu kufanyika kwa mazishi ya marehemu mbunge wa Kibra Ken Okoth siku ya Jumamosi.

Mahakama hiyo imebatilisha agizo la awali lililokuwa limesitisha kuzikwa au kuchomwa kwa mwili wa Okoth. Hii ni baada ta mlalamishi Anne Thumbi anayedai kumzalia Okoth mtoto wa kiume kuafikiana na familia ya mwenda zake na sasa mipango ya mazishi itaendelea kama ilivyokuwa imepangwa.

Mawakili Danstan Omari na Elkana Mogaka wanaomwakilishi Thumbi walisema kwamba walikuwa na mashauriano usiku kucha na familia kabla ya kuafikiana.  Pande hizo ziliafikiana kwamba uchunguzi wa DNA utafanyika na kwamba mtoto anayedaiwa kuwa wa Okoth atakuwa radhi kuhudhuria mazishi yake.

Wakili wa familia ya Okoth Edwin Sifuna siku ya Ijumaa alikuwa amesema kwamba Thumbi awali alikataa mwanawe kufanyiwa vipimo vya DNA kabla ya mbunge huyo kufariki. Thumbi aliambia gazeti la the Star kwamba ingawa hangependa kutoa maelezo zaidi kuhusu uhusiano wake na Okoth hana hofu yoyote kwamba marehemu ni babake mwanawe wa kiume.

"Bado naomboleza. Siko katika hali ya kuzungumzia chochote kuhusu swala hili. Kama unavyo fahamu swala hili liko mahakamani. Lakini niko kwa DNA ikiwa watu, wakiwemo familia ya Okoth wanashauku,” mwakilisi wadi huyo maalum alisema.

Alitaka familia imhusishe yeye na mwanawe katika mipango ya mazishi na tamaduni zote hadi kufanyika kwa mazishi yake.  Katika ombi lake mahakamani Thumbi anasema kwamba alikutana na Okoth mwaka 2013 akifanya kazi na Sonko Rescue Team na miaka miwili baadaye walibarikiwa na mtoto wa kiume.

Pia aliwasilisha picha za mamake Okoth, Angelina akiwa na mjukuu wake katika moja wepo wa nyakati walizokutana. Pia aliwasilisha picha za marehemu mbunge huyo akiwa amebeba mwanawe mabegani akiwa amejawa na furaha. Thumbi pia alitoa cheti cha kuzaliwa cha mwanawe kinachoonyesha kwamba jina la pili la mwanawe ni Okoth.

Mbali na haya yote ameonyesha ujumbe mfupi wa simu aliokuwa amemtumia Okoth akimuita “Ken Love”.

Katika ujumbe mmoja, anauliza mbunge huyo kuhusu hali yake na kuongeza kuwa, " Asante kwa baiskeli, likizo hii,  Imesaidia sana.”

Akijibu, Okoth anatuma ishara ya kucheka baada ya kumtumia picha ya mtoto akiendesha baiskeli ambayo alikuwa amemnunulia. Thumbi anasema kwamba Okoth alikuwa baba mzuri na hakusita kuajibikia majukumun ya mwanawe na kufikia kifo chake alikuwa akigharamia mahitaji ya mwanawe.