Kenya haijapiga marufuku safari za ndege kutoka Tanzania

ndege
ndege

Waziri wa uchukuzi nchini Kenya James Macharia amekanusha uwepo wa mzozo wowote wa kidiplomasia na Tanzania.

Alikuwa anajibu taarifa ya nchi za Afrika Mashirika kwamba Tanzania haitaruhusu ndege za Shirika la Kenya Airways kufanya safari zake za kutoka Nairobi kwenda Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar kuanzia Agosti 1.

Bwana Macharia amesema serikali ya Kenya haijapiga marufuku safari za ndege kutoka nchi yoyote kutua kwenye ardhi yake.

Akizungumza katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta baada ya nchi hiyo kufungua anga lake kwa ndege za kimataifa, Bwana Macharia amesema kuwa ndege za Tanzania hazijapigwa marufuku.

"Hatujapiga marufuku nchi yoyote kuingia Kenya. Hatujafunga anga letu, kile tulichofanya ni kuweka hatua ya karantini kwa baadhi ya nchi kulingana na tathmini ya janga hilo," Bwana Macharia amesema.

Macharia amesema kuwa amezungumza na mwenzake wa Tanzania Mheshimiwa Isack Kamwelwe kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili na kuwa agizo la Tanzania litapitiwa tena hivi karibuni.

"Kenya haijapiga marufuku ndege kutoka Tanzania. Kenya haijapiga marufuku wasafiri kutoka Tanzania. Tulichofanya ni kuweka kanuni fulani za kiafya watu watakapowasili kutoka nchi mbalimbali," Bwana Macharia amesema.

Bwana Macharia ameongeza kwamba ndege za Kenya zitaruhusiwa kuingia katika anga la Tanzania baada ya kufikiwa kwa makubaliano.

Aidha, Bwana macharia ameongeza kuwa orodha ya nchi 19 bado inapitiwa na itaendelea kubadilika kulingana na vile nchi zitakavyoendelea kukabiliana na usambaaji wa ugonjwa wa virusi vya corona huo katika maeneo ya mipakani.

Awali, Tanzania ilipiga marufuku Shirika la ndege la Kenya Airways kufanya safiri nchini humo hadi wakati usiojulikana.

Taarifa iliyotolewa na mamlaka ya usafiri wa anga nchini humo (TCAA) ni kwamba nchi hiyo imeondoa idhini iliyopewa Shirika la ndege la Kenya Airways kuanza tena safari za kimataifa nchini Tanzania ikijubu hatua iliyochukuliwa na Kenya ya kutoijumuisha kwenye orodha ya nchi iliyotolewa.

-BBC