Kenya na Somalia zakubaliana mpango wa kutoa vyeti vya visa raia wanapowasili

kenya na somalia
kenya na somalia

Kenya na Somalia  leo zimekubaliana kulainisha uhusiano kati yao kwa  kurejesha mpango wa kutoa vyeti vya visa kwa raia wa mataifa haya mawili wanapowasili.

Kurejeshwa kwa mpango huo wa vyeti vya visa kunakusudiwa kuimarisha usafiri huru wa watu na biashara bila vikwazo kati ya Kenya na Somalia.

Mpango huo uliafikiwa leo wakati wa mkutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia pembezoni mwa Kongamano la Kimataifa linaloendelea Jijini Nairobi kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo, ICPD25.

Wakati wa mkutano huo, viongozi hao wawili walikariri  umuhimu wa uhusiano mzuri kati ya Kenya na Somalia na wakakubaliana kutafuta mbinu za kuboresha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Nairobi na Mogadishu kwa manufaa ya raia wa mataifa haya mawili.

Rais Mohamed alimpongeza Rais Kenyatta kwa wajibu ambao Kenya inaendelea kutekeleza chini ya kikosi cha AMISOM na ukarimu wake kwa wakimbizi wa Somalia.

Kiongozi huyo wa Somali alielezea matumaini yake kwamba mzozo kuhusu mpaka wa baharini kati ya Somalia na Kenya ambao sasa uko katika Mahakama ya Haki ya Kimataifa [ICJ] huko Hague utasuluhishwa kwa njia bora inayokubalika.