Kenya yafilisika, njama ya kuwafuta wafanyakazi wa umma yaelezwa

dEyuGEUf
dEyuGEUf
Serikali inatafakari kuhusu mpango wa kupunguza idadi ya wafanyikazi wa umma kama mbinu ya kupunguza matumizi ya pesa za serikali.

Tume ya kudhibiti mishahara ya wafanyikazi (SRC) imeitisha mkutano wiki ijayo kujadili mikakati inayostahili kuwekwa katika muda wa miaka mitatu ijayo ili kupunguza matumizi ya pesa serikalini.

SRC inasema hata ingawa matumizi ya pesa za serikali yamepungua kutoka asilimia 57.33 kulingana na mapato ya serikali mwaka wa kifedha wa 2013-2014 hadi asilimia 48.1 ya mapato ya kipindi cha kifedha cha mwaka uliyopita, juhudi zaidi zinafaa kufanywa kupunguza kiwango hicho hadi asilimia 35.

"Matumizi ya serikali ambayo hayaambatani na mapato ya ukuaji wa uchumi huwekea shinikizo bajeti za maendeleo na uwekezaji, kumaanisha mgao wa maendeleo na miradi ya utoaji huduma za kijamii kama vile elimu na afya utapungua," Mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich alisema.

Uamuzi wa kufanyia marekebisho matumizi ya pesa za serikali umechochewa na kupungua kwa kiasi cha pesa zinazokusanywa na mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini KRA na madeni ya kimataifa, hali ambayo imelazimisha hazina ya kitaifa kuchukua hatua madhubuti kupunguza matumizi ya pesa.

Mwezi uliopita, kaimu waziri wa Fedha Ukur Yatani alitangaza mikakati kadhaa ya serikali kupunguza gharama za kuendesha serikali. Zilihusisha kupunguza matumizi ya simu, magazeti, matangazo ya biashara, safari za kimataifa, ununuzi wa magari na kukodisha.

Alisema hatua hii ilihitajika ili kufanikisha ajenda kuu nne za serikali (Big Four Agenda) ,shinikikizo katika matumizi ya fedha za umma, kupungua kwa mapato ya serikali na kiasi cha juu cha mikopo ya serikali.

“Hatunabudi ila kudhibiti gharama za kuendesha serikali," alisema.

Siku ya Jumatano, SRC ilisema kwamba kutokana na shinikizo za gaharama za kuendesha sekta za umma, serikali inafaa kuboresha mipangilio yake ya kifedha.

Waziri wa utumishi wa umma Margaret Kobia hata hivyo alipuuzilia mbali, kuachishwa watu kazi kama hatua ya kupunguza matumizi ya pesa za serikali, akisema kwamba wakati wa kongamano lao watapendekeza kupunguza wafanyikazi kwa kutojaza nafasi za wafanyikazi wanaostaafu au kufariki.

“Kustaafisha watu mapema sio njia mwafaka. Tulijifunza kutokana na hatua kama hiyo iliyofanyika mwaka 2000. Ukiachisha watu kazi unaongeza viwango vya ufukara. Tunaweza kuamua kutojaza nafasi za wale wanaostaafu au kukataa kuwapa kandarasi mpya wale ambao kandarasi zao zimekamilika” Kobia alisema.