Khaligraph Jones, aelezea sababu ya kutema mziki wa dini

Je wafahamu kwamba takriban muongo mmoja uliopita, Khaligraph Jones alikuwa mwanamziki wa nyimbo za kumtukuza mwenyezi Mungu?

“Mwaka 2009, nilianza kuimba kama mwanamziki wa kulipwa, baada ya kushiriki mashindano ya mziki wa kufoka au rap kwa Channel O na kushinda, lakini sikuwa na kitambulisho au paspoti kwa sababu nilikuwa katika shule ya upili,” Khaligraph Jones alisema.

Aliendelea,

“Hata ingawa nilianza nyimbo za kufoka (rapping) nikiwa mtoto. Nilianza mziki wa dini mwaka 2004, nilirekodi wimbo wangu wa kwanza na Hope Kid - na hata tukaunda kikundi. Hata hivyo mara ya kwanza nilipanda jukwaani kama  KHALIGRAPH JONES ilikuwa mwaka 2008 katika studio za WAPI (WORDS AND PICTURES). Hapo ndipo nilizindua taaluma yangu ya mziki na kuachilia mziki wa injili.”

Kuhusu sababu za kuacha nyimbo za dini, Khaligrapg alisema'

“Nilitaka kufanya kitu nitakacho na sio kwa kulazimishwa. Nilitaka kujitengenezea njia yangu. Wakati huo mahali nilitoka kila mtu alikuwa anafanya mziki wa kumtukuza Mungu. Lakini mimi mwenyewe sikuridhika na sikutaka kuwaambia watu waishi maisha ambayo mimi mwenyewe sikuyaishi.”

Khaligraph aliongeza,

“Sikutaka kuhubiri maji nami mwenyewe nanywa mvinyo. Ikiwa utafika wakati nitapata mwito kumhudumia Mungu, basi bila shaka nitaitika .”