Kifo cha Ghafla: Waziri Mkuu wa Ivory Coast Gon Coulibaly aaga dunia baada ya mkutano wa baraza la mawaziri

Waziri Mkuu wa Ivory Coast Amadou Coulibaly amefariki baada ya kuugua wakati wa kikao cha baraza la mawaziri.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 61 alikuwa amechaguliwa kuwa mgombea wa chama tawala katika uchaguzi wa mwezi Oktoba, baada ya Alessane Ouattara kusema kuwa hatowania muhula wa tatu.

Bwana Gon Coulibaly alikuwa amerudi kutoka Ufaransa ambapo alikuwa amepokea matibabu ya moyo kwa miezi miwili.

Rais Ouattara amesema kuwa taifa linaomboleza.

Alisema kwamba bwana Gon Coulibaly alianza kuhisi vibaya wakati wa kikao cha kila wiki cha baraza la mawaziri na akapelekwa hospitali ambapo alifariki baadaye.

Kifo chake  huenda kitasababisha hali ya wasi wasi  kuhusu uchaguzi huo.

Bwana Coulibali alifanyiwa upandikizaji wa moyo 2012 na alikuwa ameelekea Ufaransa tarehe 2 Mei ili kuwekewa bomba katika mshipa wake wa damu.

Alirudi Alhamisi iliopita na kusema: Nimerudi kuchukua mahala pangu kando ya rais , ili kuendelea na jukumu la kujenga taifa letu.

Taarifa moja katika gazeti la Le Monde siku ya Jumatatu ilimnukuu afisa mmoja wa kigeni ambaye yumo nchini humo kama mchunguzaji wa uchaguzi huo ilisema: Iwapo Gon Coulibaly hajapona, Ouattara atakuwa hana chaguo bali kuwania kwa muhula mwengine kwasababu hakuna mpango mwengine.

Suala hili kufikia sasa limekuwa mwiko kwasababu rais amesema yuko tayari kuondoka na kutaja ni nani chaguo la mtu atakayemrithi.

Chaguo la bwana Ouattara kutowania urais mwezi Machi lilishangaza taifa hilo.