Kilichofanyika ni kipi? Baada ya kuishi pamoja kwa miezi 6, mbona ghafla Vigilance Shighi akaamua kumuua Okello?

Vigilance Shighi, 29 sasa yupo seli  na atasalia huko kwa siku 21 zijazo huku polisi wakiendelea kuchunguza hali iliyosababisha  kifo cha mpenzi wake mhandisi  Edward Okello mwenye umri wa miaka 33.

Wawili hao walikuwa wameishi pamoja kwa miezi sita pekee na wengi wanajiuliza maswali ya kilichosababisha Shughi kuamua kuchukua kisu na kumdunga Okello wakiwa katika nyumba yao mtaani Umoja. Shighi anasema alimtupia kikombe Okello walipogombana na  kuanzia hapo hajui kilichofanyika. Baada ya kumdunga kisu, inadaiwa Shighi alikimbia nje kuwaita majirani wampe usaidizi ili kumpeleka Okello katika hospitali ya Mama Lucy. Kwa bahati mbaya, alikata roho alipokuwa anatibiwa katika hospitali hiyo. Tukio hilo baadaye liliripotiwa katika kituo cha polisi cha Buruburu.

Polisi walipofika katika eneo la mkasa waliweza kupata kisu cha jikoni kilichokuwa  kimelowa damu  na kinachoaminika kutumiwa katika mauaji ya Okello. Je, kilichosababisha mauaji hayo ni kipi? Kachero Veronicah Waithera amesema uchunguzi bado haujakamilishwa  na anahitaji muda kuzichunguza simu za marehemu na pia  kuwahoji mashahidi. Waithra pia anasema  mwili wa marehemu haujafanyiwa uchunguzi ilhali mshukiwa pia anafaa kufanyiwa uchunguzi wa kiakili. Shighi amekana kumuua mpenzi wake  na upande wa mashtaka unahofu kwamba huenda  angetoroka endapo angeachiliwa huru.

“ Mheshimiwa jaji, tuligombana nikamtupia kikombe lakini sikumuua ..mimi sio muuaji.’ Shughi alimuambia jaji .

Jaji Gatheru alimwambia kwamba anachunguzwa wala hajashtumiwa kwa mauaji ya mpenzi wake. Kesi hiyo itatajwa Juni tarehe 2.