KISUMU: Meneja wa hoteli amuua mwanaume kwa kumpiga risasi

meneja
meneja
Mtu mmoja alipigwa risasi na kuuawa mjini Kisumu siku ya Jumamosi.

Peter Otieno Ogallo alipigwa risasi tatu kifuani na Daniel Yona Jaoko, meneja wa hoteli ya Ray Green mjini Nyamasaria.

Otieno ambaye ni meneja wa Coast Bus tawi la Kisumu, alipigwa risasi mbele ya familia yake na akakimbizwa katika hospitali ya Avenue ambapo alifariki.

Jaoko alikuwa tu amemfikisha mpenziwe Vivian Achieng Meresa ambaye anaishi mtaa moja na marehemu wakati wa kisa hicho cha saa kumi na moja asubuhi katika  eneo la Polyview.

Kamishna wa polisi wa kaunti ya Kisumu Benson Maweu alisema kuwa Jaoko na Vivian wametiwa mbaroni kuhusiana na mauaji hayo.

Maweu alisema kuwa marehemu alipigwa risasi akijaribu kuondoa gari lake la Nissan matatu la usajili KCU 552X ambapo lilikuwa limeegezwa.

Gari la Otieno lilikuwa limezibwa na gari lingine la aina ya Jeep la usajili KCC 422T. “Alipomkaribia Jaoko kumpisha apite ili aondoe gari lake, lakini badala atoe gari alitoa bastola na kumpiga risasi." Alisema Maweu.

Maweu aliambia The Star kupitia simu kuwa risasi mbili ziliingia katika upande wa kushoto wa kifua cha Otieno na kuharibu mapafu yake.

Washukiwa hao wamezuiwa katika kituo cha polisi cha Kondele. Mkuu wapolisi alisema kuwa swala hilo bado linachunguzwa.

"Tutawafikisha kortini pindi tu uchunguzi utakapo kamilika." Aliongeza.

Maweu alisema kuwa walipata bunduki aina ya Ceska lenye risasi 15 walipo wakamata washukiwa hao wawili huku risasi zingine 42 zikipatikana nyumbani kwake Jaoko.