Kivumbi baina ya Ruto na Gideon huku Gideon akimrithi babake

Kivumbi cha kisiasa kinatarajiwa katika Bonde la Ufa baada ya Seneta wa Baringo Gideon Moi kupewa idhini na familia yake kuongoza familia hiyo katika ulingo wa siasa.

Moi na naibu rais William Ruto wamekuwa wakipigana kumbo kuona ni nani ana ushawishi wa kisiasa katika jamii ya Kalenjin na sasa baada ya Gideon kupokezwa rungu ya mamlaka ya marehemu babake nyasi zitaumia.

Seneta wa Baringo Gideon Moi siku ya Jumatano alipokezwa rungu ya babake, ishara kuwa yeye ndiye aliyeteuliwa na hayati Rais mustaafu Daniel Moi kuwa mrithi wake wa siasa.

Ilitangazwa pia hadharani kuwa marehemu rais Mustaafu Daniel Moi alikuwa ametaja kitinda mimba wake Gideon Moi kuchukuwa usukani wake katika ulingi wa siasa.

Jamaa wa karibu na familia ya Moi walieleza Radio Jambo kuwa marehemu Moi aliambia familia yake yote, miaka kadhaa kabla ya kifo chake kwamba Gideon Moi alikwa chaguo lake kama mrithi wake.

Kisha alianza kumpa mwelekeo katika ulingo wa kisiasa alipokuwa anaanza safari yake ya siasa.

"Ni hayati Moi aliyemshinikiza Gideon kujiunga na siasa. Seneta huyo hakutaka kujiunga na siasa kwa sababu alikuwa na mipango mingine, lakini babake alisisitiza kwamba ilikuwa lazima agombee wadhifa wa kisaiasa na kuchukuwa usukani wa kuongoza chama cha KANU.

"Hata baada ya kujiunga na siasa, babake aliendelea kumpa muongozo kuhusu njia ya kufuata na viongozi wa kushirikiana nao ili kujijenga kisiasa. Kila mtu katika familia alijua," duru ilisema.

Hatua ya Gideon kuungwa mkono na familia yake sasa huenda ikazua kivumbi cha kisaiasa baina yake na naibu rais William Ruto, huku wakipigania ubabe katika eneo la Bonde la Ufa.

Kulingana na mila za jamii ya Kalenjin, kakake mkubwa aliyepo sasa Raymond Moi alistahili kupokezwa rungu ya uongozi.

Uamuzi huo umemaliza uvumi kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwa wanawe wa kiume wa marehemu rais Moi kuhusu mrithi wa mali yake ya mabilioni ya pesa huku ikidaiwa kwamba Gideon alikuwa amependelewa sana na mzee Moi.