Kivumbi cha BBI: Huenda Ruto na Raila wakakutana kwenye jukwaa la BBI Mombasa

Huenda naibu rais William Ruto na Kinara wa upinzani Raila Odinga wakakutana katika jukwaa moja kupigia dembe mchakato wa BBI.

Katika mahojiano kwenye kituo kimoja cha televisheni nchini naibu rais William Ruto alisema kwamba huenda akajiunga na wanasiasa wengine katika mkutano wa BBI mjini Mombasa siku ya Jumamosi ikiwa ataambiwa na rais Uhuru Kenyatta kuhudhuria mkutano huo.

Wanasiasa wanaomuunga mkono Ruto mapema wiki hii walitangaza kubadili msimamo wao kuhusu mikutano ya kupigia debe mchakato wa BBI na kuahihidi kuhudhuria mkutano wa Mombasa na mikutano mingine itakayofuata.

Katika mahojiano ya jana, Ruto alisema mchakato wa BBI haufai kutekwa nyara na kundi moja la wanasiasa bali unafaa kumilikiwa na wakenya wote. Alidai kuwa asilimia 90 ya watu ambao wamekuwa wakihudhuria mikutano ya BBI ni wafuasi wa ODM huku lengo lao likiwa kutumia fursa hiyo kuanza kampeni za mwaka 2022.

Kuhusu hali ya chama tawala cha Jubilee, Ruto alionekana kukashifu usimamizi wa chama hicho akisema kwamba chama hicho hakija andaa mkutano wowote kwa miaka miwili sasa. Licha ya kukiri kuwepo kwa changamoto naibu rais alikanusha kuwepo kwa mgawanyiko chamani.

Ruto ambaye pia ni naibu kinara wa Jubilee alisema kwamba chama hicho kitaanda uchaguzi wa maafisa wake wapya mwezi Machi mwaka huu.

Wakati huo huo naibu rais anadai kuwepo kwa njama ya kufufua kesi dhidi yake katika mahakama ya uhalifu wa kimataifa ICC.

Akizungumza katika mahojiano kwenye kituo cha televisheni nchini Ruto alisema kwamba mkuu wa idara ya ujasusi nchini – NIS, alimweleza kuwa tayari kuna makachero waliotumwa nchini kwa lengo la kufufua kesi iliyokuwa ikimkabili katika mahakama ya kimataifa ICC.

Naibu rais alidai kwamba sababu kuu ya kurejelea kesi za ICC ni kumzuia asiwaniye urais katika uchaguzi mkuu mwaka 2022.

Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walikuwa wameshtakiwa katika mahakama ya ICC wakikabiliwa na tuhuma za mauaji na dhulma dhidi ya binadamu Kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007/2008.

Zaidi ya watu elfu moja waliuawa na mamia ya maelfu kufurushwa makwao kutokana na ghasia hizo. Kesi dhidi yao na wakenya wengine wanne hata hivyo zilitupiliwa mbali kutokana ukosefu wa mashahidi.

Wakati huo huo naibu rais alipuuzilia mbali madai ya kuwepo kwa uhasama baina yake na rais Uhuru Kenyatta. Alisema ana uhusiano mwema na rais Kenyatta na kumpuuzilia mbali kinara wa upinzani Raila Odinga kwa kujifanya sasa kuwa mwandani wa Uhuru na ilhali alikuwa akimkashifu.

Ruto amekuwa katika mstari wa mbele kupinga salamu za maridhiano baina ya rais Kenyatta na Raila Odinga.  Naibu rais alisema hakuna mwanasiasa humu nchin ambaye ameunga uhuru mkono kumliko yeye.

“Nimemuunga mkono sana Uhuru, hata wakati kila mwanasiasa alijitenga naye, mwaka 2002 nilimpigia debe sana na hata kushinikiza atangaze kukubali matokeo ya uchaguzi mwaka 2002, ilipoomekana wazi kwamba Mwai Kibaki wa Narc alikuwa amezoa kura nyingi,?” Ruto alisema.