Kizimbani! Aisha Jumwa aachilwa kwa dhamana

jumwa
jumwa
Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mlinzi wake Okuto Otieno wameachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja na mdhamini wa kiasi sawa na hicho au pesa taslim shilingi laki tano.

‘Wawili hawa wataachiliwa lakini lazima wajiwasilishe kwa idara ya DCIO Malindi tarehe 22, Oktoba…maagizo mengine ya ziada yatatolewa,” Hakimu mkuu mkaazi Vincent Adet alisema siku ya Alhamisi.

Adet alisema polisi watakuwa huru kuwashtaki wawili hao punde tu watakapopata ushahidi dhidi yao.

"Ni kinyume cha sheria kwa polisi kuendelea kumzuilia mtu wasiyekuwa na ushahidi kuwezesha kumfungulia mashtaka. Katiba inapinga hili," Alisema.

Jumwa na mlinzi wake, Okuto otieno, walikesha katika seli za polisi wakisubiri kufikiwa mahakamani siku ya Alhamisi.

Ajali inayohusisha magari manane yasabisha msongamano Nairobi

Wawili hao walipelekwa katika kituo cha polisi cha mahakama.

Upande wa mashtaka ulikuwa umeomba mahakama iwazuiliye kwa siku 21 kupata muda wa kutosha kukamilisha uchunguzi.

Jumwa alikamatwa pamoja na Otieno na wafanyikazi wake wengine wawili baada ya mtu mmoja kuauwa kwa kupigwa risasi siku ya Jumanne.

Mwanamume Ngumbao Jola alipigwa risasi na kufariki baada ya rabsha kuzuka katika boma la mgombeaji wa ODM  katika uchaguzi mdogo wa eneo la uakilishi wadi la Ganda, Reuben Katana.

Ghasia hizo zilianza baada ya Jumwa kuvamia boma la Katana kutatizo mkutano uliokuwa ukiendelea baina ya Katana na maajenti wake wa ODM wakitayarishwa kwa uchaguzi mdogo wa siku ya Ijuma.

Aisha alidai kuwa mgombeaji huyo alikuwa anafanya kampeni baada ya kukamilika kwa muda rasmi wa kufanyika kwa kampeni.